Jamii FM
Jamii FM
16 December 2025, 16:59 pm

Ujenzi wa kiwanda cha Tells One General Supply Mahuta wilayani Tandahimba mkoani Mtwara umeleta faraja kwa akina mama na wabanguaji wadogo wa korosho. Kiwanda hicho kimewezesha upatikanaji wa soko, ajira na kuboresha maisha ya wananchi hususan wanawake wa eneo hilo
Na Musa Mtepa
Vikundi vya akina mama na wabanguaji wadogo wa korosho Mahuta wilayani Tandahimba mkoani Mtwara vimeeleza kufurahishwa kwao na ujenzi wa kiwanda pamoja na kituo cha kuwasaidia kupata soko na ajira cha Tells One General Supply.
Wakizungumza kuhusu manufaa wanayoyapata kutokana na uwepo wa kiwanda hicho, Bi Amina Mande na Bi Amina Makwangu, ambao ni wafanyakazi wa kiwanda hicho, wamesema kuwa kiwanda kimekuwa msaada mkubwa katika kutatua changamoto zao za kimaisha ikiwemo kusomesha watoto na kujikimu katika mahitaji ya kila siku.

Kwa upande wake, msimamizi wa kiwanda hicho, Bi Mariamu Chilongo, amesema dhamira ya kuanzishwa kwa kiwanda hicho ni kuwasaidia wabanguaji wadogo wa korosho, hususan akina mama, ambao hapo awali walikuwa wakikumbana na changamoto ya upatikanaji wa masoko. Amesema kiwanda hicho hupokea korosho zilizobanguliwa, kuziboresha na kuzisafirisha kwenda sokoni.

Aidha, Bi Mariamu amesema kuwa pamoja na kupokea korosho kutoka katika vikundi mbalimbali, kiwanda hicho tayari kimeajiri wafanyakazi wa kike wasiopungua 50, huku matarajio yakiwa ni kuongeza idadi hiyo hadi kufikia wafanyakazi 500 siku za usoni.
Sauti ya Bi Mariamu Chilongo, Msimamizi wa Kiwanda
Kituo na kiwanda cha Tells One General Supply (TOGS) kimejengwa katika kijiji cha Mahuta wilayani Tandahimba mkoani Mtwara, kikiwa na lengo la kusaidia upatikanaji wa soko la korosho kwa vikundi vidogo vya ubanguaji pamoja na kutoa ajira kwa akina mama wa eneo hilo.
