Jamii FM
Jamii FM
16 November 2025, 15:37 pm

Wafanyabiashara wa Mtwara wamelalamikia ongezeko la tozo na ushuru linalodaiwa kupandisha bei za bidhaa, huku wakitaka serikali kupitia upya kanuni hizo. Manispaa imesisitiza kuwa tozo zinatekelezwa kwa mujibu wa sheria na iko tayari kushughulikia malalamiko kupitia majadiliano
Na Musa Mtepa
Wafanyabiashara mjini Mtwara wamelalamikia ongezeko la ushuru unaoendelea kutungwa katika biashara zao, wakieleza kuwa hatua hiyo inaathiri bei za bidhaa na kuhatarisha uwezo wa mlaji wa mwisho kumudu bidhaa hizo.
Wakizungumza Novemba 15, 2025 katika mkutano wa Ushirika wa Wafanyabiashara (WABISOKO) uliofanyika katika viwanja vya Mashujaa, Manispaa ya Mtwara Mikindani, wafanyabiashara hao wamesema mkutano huo umewezesha kutoa taarifa za maendeleo ya ushirika pamoja na changamoto zinazowakabili.
Akielezea hali ya tozo wanazokutana nazo wanapoingiza bidhaa ndani ya manispaa, Selemani Kadege amesema kuwa endapo serikali haitapitia upya ushuru unaotozwa, bidhaa zitaendelea kuwa ghali na hivyo kumuumiza mlaji wa mwisho.
Kwa upande wake, Asha Abilahi, mfanyabiashara wa Soko la Chuno, amesema kuwa wamekuwa wakitozwa ushuru katika vizuizi vya barabarani, ambapo baadhi ya watendaji hawatoi risiti, hali ambayo imekuwa kero kwao. Ameiomba serikali kufuatilia suala hilo kwa umakini zaidi.
Aidha, Bi. Asha ameiomba serikali kuhakikisha wafanyabiashara wakubwa wa vyakula, minada na nguo wanapelekwa Soko la Chuno ili kulihuisha na kuongeza mzunguko wa biashara, badala ya wafanyabiashara kufanyika nje ya eneo la soko hilo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu tozo hizo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Rugembe Maiga amesema kuwa ushuru unaotozwa unatokana na sheria iliyopitishwa kwa kuzingatia taratibu. Ameongeza kuwa iwapo kuna malalamiko au changamoto, manispaa ipo tayari kukaa na wafanyabiashara kupitia maeneo yenye matatizo.
Amesisitiza kuwa kwa sasa sheria tayari imetungwa, hivyo wafanyabiashara wanapaswa kuendelea kulipa kodi, ada na ushuru kwa viwango vilivyowekwa mpaka pale maboresho yatakapofanyika na kupitishwa na mamlaka husika.
