Jamii FM

Mtwara kutenga milioni 500 kuboresha Soko Kuu

16 November 2025, 15:23 pm

Bw. Rugembe Maiga akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri ya Manspaa ya Mtwara Mikindani katika mkutano wa WABISOKO(picha na Musa Mtepa)

Manispaa ya Mtwara–Mikindani imetangaza mpango wa kutenga zaidi ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuboresha Soko Kuu la Mtwara, ikilenga kuboresha miundombinu na mazingira ya biashara huku wafanyabiashara wakiyakaribisha maboresho hayo na kuomba kupewa kipaumbele baada ya ujenzi kukamilika

Na Musa Mtepa

Zaidi ya shilingi milioni 500 zinatarajiwa kutengwa kwa ajili ya kuanza mchakato wa uboreshaji wa ujenzi wa Soko Kuu la Mtwara, hatua inayolenga kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika mazingira bora na yenye hadhi inayolingana na Manispaa ya Mtwara–Mikindani.

Akimwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara–Mikindani kwenye mkutano wa Ushirika wa Wafanyabiashara wa Soko Kuu (WABISOKO) uliofanyika Novemba 15, 2025 katika Viwanja vya Mashujaa, Bw. Rugembe Maiga amesema kuwa pamoja na jitihada nyingi zilizofanywa na serikali, bado wanatambua kuwa soko hilo ni chakavu na linahitaji maboresho ili liendane na hadhi ya manispaa.

Sauti ya Rugembe Maiga, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara–Mikindani

Aidha, Bw. Rugembe amesema kuwa mbali na mipango ya ujenzi mpya, tayari wameanza kushughulikia baadhi ya changamoto zilizokuwa zikiwakabili wafanyabiashara ikiwemo uboreshaji wa huduma za choo, maeneo ya kufanyia biashara pamoja na mitaro ya kupitisha maji.

Sauti ya Rugembe Maiga, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara–Mikindani

Wakizungumzia mpango huo, wafanyabiashara wa soko hilo, Selemani Kadege na Ramadhani Mtumba, wameishukuru serikali kwa hatua hizo za maboresho, huku wakitoa ombi la kupewa kipaumbele wafanyabiashara waliopo sasa mara baada ya ujenzi kukamilika.


Sauti ya Selemani Kadege na Ramadhani Mtumba – Wafanyabiashara