Makala: Changamoto zinazokwamisha wanawake kushiriki uongozi
16 November 2024, 15:42 pm
Na Mwanahamisi Chikambu na Gregory Millanzi
Ushiriki wa wanawake katika uongozi ni hatua muhimu kuelekea usawa katika uongozi na maendeleo ya kijamii. Hata hivyo uwakilishi wa wanawake katika nafasi za uongozi bado ni mdogo na changamoto mbalimbali zinakwamisha juhudi za kufikia usawa huu.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mihambwe, Kata ya Naliendele, Brandina Chilumba amesema kuwa moja ya changamoto kuu ni ukosefu wa kujiamini miongoni mwa wanawake. “Wanawake wakijiamini wanaweza, kwani kazi ya uongozi huifanyi peke yako, unashirikiana na wananchi na mimi wananipa ushirikiano na wananchi wananipenda,” amesema Chilumba.
Kwa upande wake, Shamsia Manka, Diwani wa Viti Maalum wa tarafa ya Mpapula, ameeleza kuwa changamoto ya mfumo dume ni kikwazo kikubwa kwa wanawake kuingia katika nafasi za uongozi. Mfumo huu umekuwa ukikandamiza wanawake na kuwanyima nafasi ya kushiriki kikamilifu katika masuala ya maendeleo.
Katika mjadala huu, mratibu wa shirika la FAWOPA, Justine Kabelege, ameweka wazi changamoto wanazokumbana nazo wanawake, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa fursa na unyanyapaa wa kijinsia. Hata hivyo, ameainisha juhudi mbalimbali zinazofanywa na shirika hilo ili kuwawezesha wanawake kuingia katika uongozi na kufanikisha malengo yao.