Wazazi kikwazo watoto kumaliza elimu ya msingi Mtwara DC
16 April 2024, 08:55 am
Wazazi wengi wamekuwa wakiweka nguvu kubwa kwenye mila ya Jando na unyango kuliko Elimu
Na Musa Mtepa
Inaelezwa kuwa Wazazi kutotambua umuhimu wa Elimu ndio chanzo cha Watoto wengi kutomaliza Elimu ya Msingi katika Halmashauri ya Mtwara Vijijini.
Wakizungumza na Jamii Fm Radio Wananchi wa kata ya Mkunwa Halmashauri ya Mtwara vijijini mkoani Mtwara wamesema kuwa Wazazi wengi wamekuwa wakiweka nguvu kubwa kwenye mila ya Jando na unyango kuliko Elimu.
Bi Stella Kasiani Mzazi na mkazi wa Kijiji cha Mkunwa amesema kumekuwa na tabia ya Wazazi kuwapeleka Watoto Jandoni kipindi ambacho bado masomo yakiwa yanaendelea huku akiiomba Serikali kuweka sheria na kuwachukulia hatua kwa Wazazi wenye tabia kama hiyo.
Aidha Kwa upande wa Bakari Hamisi mkazi wa kjiji cha Miwindi ameziomba serikali za Vijiji Kusimamia na kuthibiti ufanyikaji holela wa Mila za jando za unyago ili kuwaokoa Watoto wanaokosa Masomo wakiwa kwenye sherehe hizo.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa kata ya Mkunwa Aroun Parselaw amesema kuwa ili kukabiriana na chanagamoto hiyo wao kama serikali ya kata watapanga ratiba na utaratibu rafiki juu ya sherehe za jando na unyago kufanyika kwa tarehe maalumu itakayopangwa.