Namtumbuka atahadharisha matumizi mihuri kinyume na utaratibu
15 December 2024, 11:24 am
Ni kikao kazi kilichoitishwa na Diwani wa kata ya Namtumbuka Al-haji Salumu Lipwelele kwa viongozi wa vijiji waliochaguliwa hivi karibuni chenye lengo la kufahamiana na wakuu wa idara waliopo katika kata ya Namtumbuka ili kurahisisha katika utekelezaji wa majuku yao.
Na Musa Mtepa
Katibu wa Siasa na Uenezi CCM wa kata ya Namtumbuka, Musa Halfani Namkopa, amewataka wenyeviti wa vitongoji na vijiji kushirikisha wajumbe wa serikali za vijiji kwenye miradi na shughuli za maendeleo zinazofanyika katika vijiji vyao, pamoja na matumizi ya rasilimali za ofisi.
Namkopa amesema hayo kwenye kikao cha kazi cha viongozi wa vijiji sita wa kata ya Namtumbuka Halmashauri ya Mji Nanyamba Mkoani Mtwara ,kilichofanyika Disemba 10, 2024, katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Sekondari Namtumbuka,kilichokuwa na lengo la kufahamiana viongozi wa vijiji na wakuu wa idara wa kata hiyo, pamoja na kujenga ushirikiano baina yao.
Katibu Namkopa ameeleza kuwa kumekuwepo na baadhi ya wenyeviti wa vijiji wanaoingilia kazi za watendaji, akitolea mfano tabia ya kung’ang’ania matumizi ya mihuri bila kuhusisha watendaji wa vijiji.
Mwenyekiti wa CCM kata ya Namtumbuka, Issa Ntili, amesisitiza umuhimu wa viongozi wa vijiji kufanya kazi za maendeleo kwa lengo la kuleta maendeleo katika vijiji vyao na kuongeza kuwa miradi ya maendeleo inapaswa kuibuliwa na viongozi wa vijiji ili Diwani aweze kuwasilisha na kupigania miradi hiyo kwenye mabaraza ya madiwani.
Ntili pia amewataka viongozi wa vijiji kuachana na tabia ya kutengeneza mihuri binafsi kwa ajili ya kuandika hati na kujiingizia fedha kinyume na utaratibu na kusisitiza kuwa viongozi wanapaswa kufuata miongozo inayotolewa na serikali na kuwashirikisha watendaji wa vijiji.
Aidha, ametoa wito kwa wakuu wa idara kata ya Namtumbuka, akiwemo Afisa Kilimo, Mifugo, na Elimu, kutengeneza ushirikiano na viongozi wa vijiji kwa kushiriki katika mikutano ya vijiji ili kutoa elimu kwa wananchi na kutatua changamoto zinazowakabili.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Majengo, Abdukahar Mbaruku, ameeleza kuwa matumizi ya mihuri kinyume na utaratibu husababisha shida kwa watendaji, hasa wanapoulizwa na wakubwa wao.
Viongozi wa vijiji, Jahida Goa mjumbe wa serikali ya Kijiji cha Likwaya na Awadhi Lipipa Mwenyekiti wa Kijiji cha Majengo, wamesema kwamba suluhisho la migogoro inayosababishwa na matumizi ya mihuri ni kuwakutanisha wenyeviti na watendaji wa vijiji ili kuweka mikutano ya pamoja kuelekezana na kubaini majukumu ya kila mmoja.