Dkt. Serera aitaka CBT kuimarisha ubora wa korosho kwa soko la kimataifa
15 September 2024, 11:58 am
Soko bora la korosho huchangiwa na ubora wenyewe wa korosho hivyo wadau hawana budi kuhakikisha korosho zinazo kusanywa,kuhifadhiwa na kusafirishwa nje ya nchi zinakuwa bora kimataifa.
Na Musa Mtepa
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Ushirika na Umwagiliaji, Dkt. Suleiman Serera, ameitaka Bodi ya Korosho Tanzania na bodi ya usimamizi wa stakabadhi za ghahala kushirikiana kuhakikisha korosho zinazo kusanywa, kuhifadhiwa na kusafirishwa nje ya nchi inakuwa na ubora unaokubalika kimataifa.
Dkt. Serera amesema hayo September 13, 2024 katika kikao cha kujadili mfumo wa ununuzi wa korosho na utaratibu wa minada kwa msimu wa mwaka 2024-2025 kilichofanyika katika ukumbi wa bodi ya korosho mkoani Mtwara.
Amesema kuwa soko zuri la bei ya korosho huchangiwa na ubora wa korosho hivyo bodi ya korosho Tanzania na bodi ya usimamizi wa stakabadhi za ghalani kushirikiana katika kuhakikisha korosho zote zinazosafirishwa nje ya nchi zinakuwa na ubora unaokubalika.
Aidha Dkt. Serera ameiomba Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania TPA kuhakikisha inafanya kazi iliyotukuka kwa kushirikiana na mamala zingine katika kuhakikisha wakala wa usafirishaji wanaleta meli kwa wakati na zenye makasha ya kutosha ili kuondoa sintofahamu iliyojitokeza msimu uliopita.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania Francis Alfred amesema katika kuelekea msimu wa korosho 2024/2025 tozo zote alizokuwa anakatwa mkulima zimewekwa kwa mnunuzi lengo likiwa ni kumpatia mkulima fedha zake kulingana na bei itakayotangazwa kwenye mnada husika ambapo mkulima atakatwa tozo moja pekee kwa ajili ya gharama za usafiri.
Naye mtendaji mkuu wa soko la bidhaa Tanzania (TMX) Bw Godfrey Marekano amesema katika kuelekea msimu wa korosho 2024/2025 wamejipanga katika kuhakikisha mfumo wa ununuiz unafanya vizuri kwa wadau wote wakiwa wanatimiza majukumu yao .
Aidha kwa mujibu wa mkurugenzi wa bodi ya korosho Tanzania mnada wa kwanza wa zao la korosho kwa msimu wa 2024/25 utarajia kuanza Oktoba 14, 2024.