Jamii FM
Jamii FM
15 August 2025, 10:42 am

Kongamano limebainisha kuwa malezi duni, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na kuiga tamaduni za kigeni vinachangia mmomonyoko wa maadili na ongezeko la ukatili dhidi ya watoto, likitoa wito kwa jamii kurejesha malezi imara
Na Musa Mtepa
Matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, kuiga tamaduni za kigeni bila kuchuja, na kuporomoka kwa mifumo ya malezi ya wazazi vinatajwa kuwa miongoni mwa sababu kuu za mmomonyoko wa maadili na ongezeko la ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto katika jamii.
Hayo yamesemwa na Bi. Nanjiva Nzunda, kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, wakati wa ufunguzi wa kongamano lililolenga kujadili hali ya mmomonyoko wa maadili na njia za kuudhibiti, lililofanyika Agosti 12, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa VETA mjini Mtwara.
Bi. Nzunda amesema kuwa kutokuwepo kwa malezi imara na uwajibikaji wa wazazi kunachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa tatizo hilo.
Aidha, akitaja taarifa za Dawati la Ustawi wa Jamii mkoani Mtwara kwa kipindi cha mwaka 2022 hadi 2025, amesema jumla ya watoto 243 waliokinzana na sheria walifikishwa mahakamani, ambapo watoto 40 waliwekwa kwenye huduma za marekebisho ya tabia na katika kipindi hicho, jumla ya kesi 3,021 za ukatili dhidi ya watoto ziliripotiwa.

Bi. Nzunda ameongeza kuwa tatizo la mmomonyoko wa maadili na ukosefu wa malezi sahihi haliwezi kutatuliwa na mtu mmoja pekee, bali ni wajibu wa kila mwanajamii kushiriki kikamilifu katika kutokomeza vitendo hivyo.
Kwa upande wake, Christine Simo, Mkurugenzi wa Shirika la Upendo Charity linalofanya kazi za kijamii wilayani Masasi, amesema kuwa kitendo cha wazazi kuwaachia watoto kulelewa na bibi zao kimekuwa kikichangia mmomonyoko wa maadili mkoani Mtwara, kwa kuwa mara nyingi sauti ya bibi haina nguvu ya kumwelekeza mtoto kama mzazi.

Bi. Simo ametoa wito kwa jamii kupata elimu ya malezi na matunzo kabla ya kuingia kwenye mahusiano, ili iwapo watapata mtoto watambue jukumu na wajibu wao wa kuhakikisha mtoto analelewa ipasavyo.
