RC Sawala awataka wananchi kutoa ushirikiano dhidi ya vitendo vya ukatili
15 May 2024, 20:00 pm
Taasisi zinazohusika na utoaji wa haki na kusimamia masuala haya kuyatendea haki ili kuendelea kumlinda mtoto na mwanamke na mtanzania kwa ujumla ili awe salama zaidi.
Na Musa Mtepa
Wananchi wameombwa kushirikiana na serikali katika kuelimisha jamii kuachana na vitendo vya ukatili, kutoa taarifa na ushirikiano wakati vitendo hivyo vinapo fanyika.
Wito huo umetolewa leo tarehe 15/5/2024 na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala kwenye maadhimisho ya siku ya familia Duniani yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya shule ya sekondari Ziwani Wilayani Mtwara ambapo amesema kila mmoja anawajibu wa kutimiza wajibu wake katika malezi ikiwa na Pamoja na kutoa huduma muhimu kwa Watoto.
Aidha mkuu wa mkoa Kanali Sawala amewaomba Waandishi wa Habari kupitia vyombo vya kuendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa malezi bora ya Watoto kwa ajili ya ustawi wa maendeleo ya taifa na familia kwa ujumla.
Pia mkuu wa Mkoa ametumia maadhimisho hayo kuwataka wananchi kujitokeza kwa uwingi katika mapokezi ya Mwenge wa uhuru unaotarajiwa kupokelewa tarehe 30/5/2024 katika Kijiji cha Mapapura kilichopo halmashauri ya Mtwara vijijini ukitokea mkoani Lindi Pamoja na kuwataka wananchi wenye sifa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Mwaka huu nchini.
Kwa upande wake afisa ustawi wa jamii mkoa wa Mtwara Bi Theresia Ngonyani amesema Pamoja na umuhimu wa familia jamii imekuwa ikikutana na changamoto nyingi ikiwepo uwepo wa talaka holela ambapo 80% ya Watoto waliohudumiwa katika Halmashauri kwa kipindi cha mwezi 1 hadi Mwezi wa 3 ,2024 wanaishi kwa bibi au jamaa wengine hali inayoonesha uwepo changamoto hiyo.
Sambamba na hilo Bi Theresia amewaeleza wazazi kuwa umri wa mwaka 0 hadi 8 mtoto ubongo wake unakuwa kwa 90% hivyo kama mzazi anatakiwa kuwekeza katika umri huo ili Watoto waweze kujipambanua , kujitafakari na kujieleza vizuri ikiwa njia ya kupunguza vitendo vya Watoto kufanyiwa ukatili bila kushirikisha wazazi wao.