Jamii FM
Jamii FM
14 July 2025, 22:16 pm

Wananchi wa Kilambo, Mtwara, wameiomba serikali kurejesha feri ya MV Kilambo ili kuondoa adha ya usafiri, gharama kubwa na hatari ya kutumia viboti vidogo kuvuka mpaka kuelekea Msumbiji
Na Musa Mtepa
Baadhi ya wananchi na watumiaji wa kivuko cha Kilambo kuelekea nchi jirani ya Msumbiji wameiomba serikali kuchukua hatua za haraka kurejesha feri ya MV Kilambo ili kuondoa usumbufu na gharama kubwa wanazokumbana nazo kwa sasa.
Wakizungumza na Jamii FM Radio, wakazi hao wamesema hali ya usafiri katika eneo hilo si ya kuridhisha, kwani hulazimika kutumia viboti vidogo kuvuka mpaka huo wa maji, ambavyo si salama na vinagharimu fedha nyingi ukilinganisha na huduma ya awali ya feri.
Ahamadi Hassani na Ahamadi Fuka, wakazi wa Kijiji cha Kilambo katika Halmashauri ya Mtwara Vijijini, wanasema kuwa kutokuwepo kwa feri hiyo kunawalazimu kutumia vijiboti vidogo ambavyo vinaweka maisha yao hatarini na kuongeza gharama ya usafiri.
Kwa upande wake, Rajabu Athumani Salumu, bodaboda kutoka kijiji hicho, ameeleza kuwa ukosefu wa chombo cha uhakika cha kusafiria umepelekea mlundikano wa mizigo na abiria, huku wengine wakilazimika kulala eneo hilo kwa zaidi ya siku tatu wakisubiri usafiri.

Fatuma Bakari, mkazi wa kijiji cha Singa kilichopo nchini Msumbiji, anasema kuwa ucheleweshaji mkubwa unaosababishwa na kutokuwepo kwa kivuko umekuwa changamoto kwa wakazi wa pande zote mbili za mpaka.

Mfaume Faila, mfanyakazi wa kampuni ya uchimbaji mafuta huko Palma, Msumbiji, ameongeza kuwa gharama ya kuvuka imepanda sana, na hali hiyo inawaathiri wafanyabiashara na abiria wa kawaida.
