

14 March 2025, 13:19 pm
Hii ni katika kuwaunganisha wasikilizaji na wadau wa redio ambao wamekuwa wakisikiliza na kuchangia mada mbalimbali katika vipindi vya Jamii FM redio
Na Musa Mtepa
Kituo cha Redio cha Jamii FM Mtwara kimetoa tuzo kwa Musa Ali Chituta kutoka kijiji cha tangazo kwa kuwa msikilizaji na mchangiaji bora wa vipindi vinavyorushwa na kituo hicho.
Tuzo hiyo imetolewa kama sehemu ya kuthamini mchango mkubwa unaofanywa na wadau na wasikilizaji wa redio ambao wamekuwa wakitumia muda wao kusikiliza na kuchangia vipindi mbalimbali.
Akizungumzia kuhusu tuzo hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii FM, Said Mussa Swalla, amesema kuanzishwa kwa tuzo hizi ni hatua muhimu katika kutambua mchango wa wasikilizaji na wadau katika maendeleo ya kituo hicho.
Swalla amesisitiza kuwa tuzo hiyo ni ya mwaka 2024, ambapo vigezo vya kupokea tuzo vilikuwa ni kupiga simu na kuchangia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika vipindi vya redio. Aliongeza kuwa muundo wa tuzo utabadilika mwaka 2025.
Kwa upande wake mdau wa Jamii FM na Meneja wa miradi ya Afrika Mashariki Peik Johansson kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Vyombo vya Habari (VIKES) nchini Finland, Peik amewapongeza wasikilizaji na wadau wa redio hiyo kwa kujitolea kutoa mchango wao.
Peik amesema kuwa mchango wa wasikilizaji unatoa tafsiri sahihi ya jina la redio, kwamba Jamii FM inahudumia jamii, na bila wao redio hiyo isingeweza kuwa na mafanikio.
Aidha, Peik amemtangaza Musa Chituta kama msikilizaji bora na mchangiaji kwa mwaka 2023/2024.
Musa Chituta ameshukuru kupokea tuzo hiyo, akisema kuwa Jamii FM ni kituo cha redio kinachohudumia jamii yake kwa ukamilifu na kwamba amefurahi kupata nafasi hiyo ya kuthaminiwa.
Ameeleza kuwa, kitendo cha kumpatia tuzo hiyo kinadhihirisha umuhimu wa wasikilizaji na mchango wao kwa redio.
Baadhi ya wadau na wasikilizaji waliohudhuria hafla hiyo wameonesha furaha yao kwa kitendo cha kutambua mchango wa wasikilizaji na wachangiaji mada katika vipindi vya redio wakiahidi kupambana kwa ajili ya kushinda tuzo hii katika awamu inayofuata.
Hafla hiyo ilikutanisha wadau na wasikilizaji kumi kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mtwara, ambapo Musa Chituta ameshinda tuzo ya jumla na kubeba redio, fulana na vifaa vingine vilivyokuwa sehemu ya tuzo hiyo.