Wazazi simamieni ndoto za watoto wa kike
14 March 2021, 18:08 pm
Shirika la Sports Development Aid (SDA) limeadhimisha siku ya Wanawake Duniani Machi 12, 2021 kwa kuandaa tamasha lililowakutanisha wanafunzi wa shule ya Msingi na Sekondari Naliendele zilizopo Manispaa ya Mtwara Mikindani Mkoani Mtwara.
Lengo la tamasha hilo likilenga kuwapa elimu mabinti kuhusu usalama wao pamoja na kuwakumbusha wazazi kuwasimamia watoto wa kike ili waweze kukamilisha ndoto zao.
Akiongea katika tamasha hilo Mkurugenzi wa shirika hilo na Meneja wa mradi wa Empowered Girls speak out Thea Swai, amesema anataka kuona watoto wa kike wengi kutoka mkoa wa Mtwara wanapata nafasi katika elimu pamoja na michezo na pia kutaka watoto hao wakike kupata nafasi sawa katika kushiriki nafasi za kijamii na wazazi kuvunja Mila na Desturi zinazomkandamiza mtoto wa kike.
Afisa Elimu Taaluma wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Renalda Tesha ambae ni mgeni rasmi, amewataka mabinti kujiamini na kujifunza kwa bidii ili kufikia malengo yao na kuondoa dhana ya kuwa mtoto wa kike hawezi.
Dada mkuu wa shule ya sekondari Naliendele Tatu Mmawiniko, ameishukuru SDA kwa kuichagua shule hiyo na kuwapa Elimu rika itakayowafanya wazidi kujitambua na kujiona wapo sawa katika kupambania fursa mbalimbali.
Katika tamasha hilo michezo mbalimbali imefanyika ikiwa ni pamoja na mpira wa miguu uliochezwa katika uwanja wa shule ya msingi Naliendele Kati ya wanafunzi wa kike wa shule ya Msingi Naliendele na shule ya sekondari Naliendele, wamechuana vikali huku ushindi ukienda shule ya sekondari kwa kuibuka washindi kwa mikwaju minne ya penati dhidi ya mikwaju miwili ya Shule ya msingi Naliendele.
Shirika wametoa zawadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Vifaa vya michezo ambavyo ni mipira, Viatu, pamoja na Daftari kwa ajili ya wanafunzi walioshiriki michezo hiyo.