Jamii FM
Jamii FM
13 December 2025, 11:55 am

Taassisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele imefanya mkutano wa mwaka na wadau wa kilimo kuwasilisha matokeo ya tafiti na kujadili mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, huku ikilenga kuongeza uzalishaji wa zao la korosho msimu ujao wa kilimo
Na Musa Mtepa
TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kituo cha Naliendele, mkoani Mtwara, imeendelea na utaratibu wake wa kila mwaka wa kukutana na wadau wa kilimo kwa lengo la kuwasilisha matokeo ya tafiti zilizofanyika kwa kipindi cha mwaka mzima pamoja na kueleza matarajio ya msimu ujao wa kilimo.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Desemba 12, 2025, Kaimu Mkurugenzi wa TARI–Naliendele, Bakari Kidunda, amesema mkutano huo umewakutanisha wadau mbalimbali wa kilimo kutoka mikoa tofauti, huku ukitoa fursa kwa wadau hao kusikiliza na kujadili kazi zilizofanywa na watafiti pamoja na mipango ya tafiti zitakazofanyika katika msimu mpya wa kilimo.
Aidha, Kidunda amesema miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka uliopita ni utafiti wa teknolojia ya matumizi ya mbolea kwenye zao la korosho. Amesema utafiti huo umefikia hatua ya mwisho na matokeo yake yanakwenda moja kwa moja kwa wakulima ili yaweze kutumika kuongeza uzalishaji wa korosho.
Pamoja na mafanikio hayo, Kidunda ameainisha mabadiliko ya hali ya hewa kuwa changamoto kubwa inayokwamisha uzalishaji wa mazao kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026. Amesema TARI–Naliendele inaendelea kufanya tafiti mahsusi zitakazosaidia wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Lazaro Maliganya, Afisa Kilimo Msaidizi kutoka Halmashauri ya Songwe, akimwakilisha Mkuu wa Idara, amesema mkutano huo umempa maarifa mapya yatakayosaidia halmashauri yao kuboresha uzalishaji, hususan katika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa iliyojitokeza katika msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026.
Maliganya amesema mabadiliko hayo yameathiri uzalishaji wa zao la korosho na kusababisha halmashauri kushindwa kufikia lengo la kuzalisha tani nane, huku wakilenga kufikia tani 15 katika msimu ujao wa kilimo.
Naye George Mbaga, Afisa Kilimo kutoka Mkoa wa Tanga, amesema mabadiliko ya hali ya hewa yameathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa zao la korosho katika mkoa huo. Hata hivyo, amesema kupitia uwasilishaji wa tafiti uliofanywa na TARI–Naliendele, wamepata mwanga wa namna ya kukabiliana na changamoto za tabianchi ili kuongeza uzalishaji.
