Jamii FM
Jamii FM
13 November 2025, 11:21 am

PPRA imeendesha mafunzo kwa makundi maalumu mkoani Mtwara kuhusu taratibu za ununuzi wa umma, yakilenga kuongeza uelewa na ushiriki wao katika zabuni za serikali. Mafunzo hayo yamezinduliwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Bi. Bahati Geuzye, na yataendelea hadi Desemba katika halmashauri zote za mkoa
Na Musa Mtepa
Mtwara, Novemba 12, 2025—Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeendesha mafunzo maalumu kuhusu taratibu za manunuzi ya umma kwa makundi maalumu yakiwemo watu wenye ulemavu, kwa lengo la kuongeza uelewa na ushiriki wao katika zabuni za serikali.
Akifungua mafunzo hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Bi. Bahati Geuzye, amesema mafunzo hayo ni fursa muhimu na ya kipekee kwa wadau kutoka makundi maalumu kujifunza kuhusu sheria, kanuni na taratibu za ununuzi wa umma.

Aidha, Bi. Geuzye amesema zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya serikali hutumika kwenye ununuzi wa umma, hivyo ni muhimu kwa wananchi wote wenye sifa kushiriki na kunufaika na miradi ya maendeleo kupitia mfumo rasmi wa serikali.
Kwa upande wake, Afisa Ununuzi kutoka PPRA, Bw. Magnus Steven, amesema mafunzo hayo yalianza Novemba 10, 2025, na yataendelea hadi mwezi Desemba katika halmashauri zote za Mkoa wa Mtwara.

Bw. Steven ameongeza kuwa lengo ni kujenga uelewa na kuimarisha uaminifu kati ya makundi maalumu na serikali, ili waweze kushiriki kikamilifu na kunufaika na zabuni mbalimbali.
Washiriki wa mafunzo hayo wamesema wamepata uelewa mkubwa kuhusu namna zabuni za serikali zinavyotangazwa na nafasi ya watu wenye ulemavu katika mchakato huo, huku wakiahidi kuwa mabalozi wa kutoa elimu zaidi kwa jamii.
