Jamii FM
Jamii FM
13 July 2025, 15:42 pm

Zitto Kabwe wa ACT Wazalendo amewahamasisha wananchi wa Mtwara kushiriki uchaguzi mkuu Oktoba 2025, akisisitiza umuhimu wa kuchagua viongozi wa chama hicho ili kuleta maendeleo.
Na Musa Mtepa
Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amewaasa wananchi wa Mtwara kushiriki kwa wingi na kikamilifu katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2025, akisisitiza kuwa ni haki yao ya kisheria.
Akizungumza Julai 12, 2025 katika viwanja vya Sinani Manispaa ya Mtwara Mikindani, katika oparesheni ya chama hicho iitwayo Maji Maji, Zitto amesema kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi ikiwemo gesi asilia na zao la korosho, lakini wananchi wa maeneo hayo bado wanaishi maisha magumu ambayo hayaendani na utajiri wa mikoa hiyo.
Aidha, Zitto ameongeza kuwa endapo wananchi wa Mtwara wataamua kuwapa ridhaa viongozi wa chama chake, watahakikisha mkoa huo unageuka kuwa kitovu cha maendeleo ya kiuchumi kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kwa kutumia bandari ya Mtwara na mpaka wa Msumbiji kikamilifu kwa maendeleo ya wananchi.
Naye Waziri Kivuli wa Uchukuzi wa ACT Wazalendo, Halima Nabalang’anya, amesema kuwa chama hicho kipo tayari kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu na kuwaomba wananchi wa Mtwara kufanya maamuzi sahihi ya kuwachagua wawakilishi wa ACT Wazalendo.

Amesema moja ya changamoto kubwa ni miundombinu ya mkoa wa Mtwara kutokulingana na kiwango cha uchumi uliopo, jambo ambalo ACT Wazalendo inalenga kulitatua iwapo itapewa dhamana ya kuongoza.
