Jamii FM
Jamii FM
12 July 2025, 13:39 pm

Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Ndumbwe, Ndugu Abdull Mahupa, amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge Jimbo la Mtwara Vijijini kupitia CUF. Ametaja afya, miradi ya maendeleo na uboreshaji wa huduma kwa wananchi kuwa vipaumbele vyake
Na Musa Mtepa
Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Ndumbwe kwa kipindi cha 2020 hadi 2025, Ndugu Abdull Mahupa, ameanza safari ya kisiasa mpya kwa kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea nafasi ya ubunge katika Jimbo la Mtwara Vijijini kupitia Chama cha Wananchi (CUF).
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hiyo, Mahupa ameeleza kuwa amesukumwa na mambo makuu manne muhimu, yakiwemo masuala ya afya, usimamizi wa miradi ya maendeleo, na kuhakikisha huduma bora kwa wananchi.
Amesisitiza dhamira yake ya kusimamia utekelezaji wa sera za afya, hususan huduma za mama na mtoto kuwa bure, pamoja na kuhakikisha kuwa miradi ya serikali na ya kijimbo inatekelezwa kwa wakati na kwa manufaa ya wananchi wa Mtwara Vijijini.
Aidha, Mahupa ameahidi kuwa iwapo atapata ridhaa ya chama na wananchi, atahakikisha CUF inakuwa na ofisi yake rasmi katika jimbo hilo, hatua ambayo itasaidia kukiimarisha chama na kuwa karibu zaidi na wanachama wake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF Wilaya ya Mtwara, Bw. John Hagala, amesema hadi kufikia Julai 11, 2025, watu wawili tayari wamechukua fomu ya kugombea ubunge kupitia chama hicho na kuongeza kuwa mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu ni Julai 15, 2025.
Naye Bi. Fatuma Mselemu, mwanachama wa CUF, ameeleza kufurahishwa na mwitikio wa wanachama wengi kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya kugombea kwa kusema hali hiyo inaonesha kuwa chama kiko hai na kinafuata misingi ya demokrasia.
