Jamii FM
Jamii FM
12 May 2025, 12:18 pm

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa na utaratibu wa kutoa pembejeo za kilimo bure kwa wakulima hasa kwenye zao la Korosho
Na Msafiri Kipila
Wakulima wa zao la korosho mkoani Mtwara wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleza mpango wa utoaji wa pembejeo bure kwa wakulima wa zao hilo.
Wakizungumza na Redio Jamii FM, wakulima hao wamesema kuwa hatua hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa gharama walizokuwa wakizipata awali katika uzalishaji wa korosho. Kais Ali Mnang’umbe amesema kuwa, pamoja na juhudi hizo za serikali, bado mfumo wa usambazaji wa pembejeo hauendani kikamilifu na mahitaji halisi ya wakulima kwa wakati husika. Ameeleza kuwa baadhi ya viuatilifu vinavyotolewa havilingani na aina ya matatizo yaliyopo mashambani kwa wakati huo.
Kwa upande wake, Sharifu Kassim, mkulima na mkazi wa Kata ya Naliendele, amesema kuwa utoaji huo wa pembejeo bure umechangia kuongeza uzalishaji wa korosho, jambo lililopelekea kuongezeka kwa mapato ya fedha za kigeni kupitia mauzo ya nje ya korosho. Ameeleza kuwa hatua hiyo pia imesaidia kupunguza uhaba wa dola nchini, tofauti na hali iliyoshuhudiwa katika baadhi ya nchi za Afrika mwaka uliopita.
Juma Mng’onye, mkulima kutoka Naliendele, ameipongeza serikali kupitia Bodi ya Korosho kwa kugawa pembejeo mapema mwaka huu. Amesema hatua hiyo imesaidia kudhibiti magonjwa ya korosho katika hatua za awali na kuongeza matarajio ya uzalishaji mzuri ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo pembejeo zilicheleweshwa.
Aidha, Juma amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha nia njema kwa wakulima, hususan wa zao la korosho, na ametoa wito kwa serikali kuendeleza mfumo huu wa kuwasaidia wakulima.