Jamii FM
Jamii FM
12 April 2026, 14:27

Jamii imetakiwa kushiriki kikamilifu kulinda watoto dhidi ya ukatili, kupitia elimu na ushirikiano wa wadau mbalimbali, ili kuhakikisha usalama wa watoto chini ya miaka 18 katika Manispaa ya Mtwara Mikindani
Na Musa Mtepa
Jamii imeaswa kila mmoja kusimama katika nafasi yake ili kuhakikisha usalama na ulinzi wa mtoto vinakuwa kipaumbele, kwa lengo la kumuweka salama dhidi ya vitendo vya ukatili na matukio hatarishi.
Wito huo umetolewa Aprili 11, 2026, katika mdahalo uliowakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo mawakala wa magari ya abiria, madereva wa bodaboda, washereheshaji wa sherehe (MC), ma-DJ na waandishi wa habari.
Mdahalo huo uliondaliwa na Idara ya Ustawi wa Jamii ya Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, ukiwa na lengo la kupunguza na hatimaye kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto wenye umri chini ya miaka 18 katika manispaa hiyo.
Wakizungumza katika mdahalo huo, washiriki wameipongeza halmashauri kwa kuandaa mdahalo huo, wakisema umewawezesha kupata maarifa muhimu ambayo wataenda kuyafanyia kazi katika shughuli zao za kila siku.
Aidha, wamesema mbali na kuwa sehemu ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu matukio hatarishi kwa watoto, wametoa wito kwa halmashauri kupitia viongozi wa mitaa kuendelea kutoa elimu kuhusu ulinzi wa watoto pamoja na vihatarishi vinavyochangia ukatili huo, ikiwemo watoto kuhusishwa katika matukio ya usiku, kuhudhuria kumbi za starehe na kushiriki shughuli za mitaani.

Akizungumzia tuhuma za baadhi ya madereva wa bodaboda kuhusishwa na matukio ya ukatili kwa watoto, Hance Bruno, dereva bodaboda kutoka kata ya Shangani, amekiri kuwepo kwa baadhi yao wenye tabia hiyo, huku akiahidi kwenda kulifanyia kazi suala hilo katika kituo chake. Pia ametoa wito kwa wazazi kuwa makini na watoto wao, hasa katika kipindi cha sikukuu.
Kwa upande wake, Fatu Issa Mapua, Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, amesema miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na matukio ya ukatili yaliyojitokeza ndani ya manispaa hiyo na kupanga mikakati ya baadaye ili kuwasaidia watoto kuwa salama katika maeneo yao.
Aidha, Bi. Mapua amesema matukio ya ukatili bado yapo katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, ndiyo maana wamekuwa wakikutana na makundi mbalimbali ili kuwapatia elimu na kuiwezesha jamii kutoa taarifa pale matukio yanapotokea. Ameongeza kwa kutoa wito kwa wananchi kwamba usalama na ulinzi wa mtoto ni jukumu la kila mmoja.
