Jamii FM
Jamii FM
12 February 2026, 10:27 am

Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Frances Alfred, ametaka wakulima walipwe kulingana na uzito uliopokelewa na wahusika wa upungufu wawajibike baada ya wakulima kulalamikia tofauti ya uzito wa mazao kati ya Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) na ghala kuu, hali inayosababisha upungufu wa malipo
Na Musa Mtepa
Wakulima wa zao la korosho wamehoji kitendo cha baadhi ya Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) kupunguza kiwango cha uzito wa korosho kilichopimwa ghalani, hali inayosababisha tofauti ya malipo baada ya korosho hizo kuuzwa katika ghala kuu.
Wakichangia katika kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na Jamii FM Radio Februari 11, 2026, wakulima hao wamesema uzito unaopimwa wanapowasilisha mzigo kwenye vyama vya msingi huwa tofauti na uzito unaokuja kuzingatiwa baadaye wakati wa malipo. Wamedai kuwa wanapohoji hali hiyo kwa makatibu wa vyama wanaambiwa inatokana na tofauti ya mizani inayotumika kupimia kwenye vyama vya msingi na ile ya ghala kuu.
Akijibu hoja hiyo mubashara katika kipindi hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Ndugu Frances Alfred, amesema mkulima anapaswa kulipwa kulingana na uzito wa korosho zilizopokelewa katika chama cha msingi, na hapaswi kupunguziwa malipo kwa sababu yoyote.
Aidha, amesisitiza kuwa iwapo kutatokea upungufu wa uzito wakati wa usafirishaji kutoka chama cha msingi kwenda ghala kuu, mhusika aliyesimamia mzigo huo anapaswa kuwajibika na kufidia tofauti hiyo, badala ya mzigo huo kuhamishiwa kwa mkulima. Ameeleza kuwa vitendo vya namna hiyo ni sawa na wizi.
Pia ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakulima kuripoti changamoto zozote wanazokutana nazo kwa Bodi ya Korosho, pamoja na kuendelea kushirikiana na maafisa kilimo katika maeneo yao ili kuhakikisha wanazalisha korosho zenye ubora na zinazoweza kupata soko lenye tija zaidi.