Zao la mwani Mtwara ladoda, wakulima walilia soko
11 October 2023, 14:34 pm
Zao la mwani limekuwa zao jipya katika mkoa wa Mtwara ambapo wanawake wanaoishi kata ya Msangamkuu wamechangamkia fursa hiyo ya kilimo cha mwani na sasa hawana soko la kuuza zao hilo.
Na Musa Mtepa
Wakulima wa zao la mwani wa kijiji cha Msangamkuu, kata ya Msangamkuu mkoani Mtwara wameiomba serikali kuwatafutia soko la uhakika la zao hilo ili waweze kupata tija ukilinganisha na hali ya soko lake kwa kipindi hiki.
Wakizungumza na Jamii FM Radio wakulima hao wamesema kuwa zao la mwani limekuwa na changamoto kubwa kwenye uzalishaji wake kuanzia hatua za awali hadi kufikisha sokoni hivyo serikali na wadau wa maendeleo hawana budi kuwatafutia masoko ya uhakika wa zao hilo walilohamasika kulima kwa wingi kwa wananchi wa kata ya Msangamkuu.
Naye diwani wa kata hiyo Mheshimiwa Hamisi Saidi Mangorosho amekiri kuwepo kwa changamoto ya soko kwa wakulima hao huku akiahidi kufanyia kazi kwa kwenda kuzungumza na afisa biashara na mkurugenzi wa halmashauri ili kuhakikisha linapatikana soko la uhakika.
Akitoa mafunzo ya kulipa thamani zao hilo mwenyekiti wa mtandao wilaya na mjumbe wa kamati tendaji TUNA ALIENCE Shabani Mayonzi amesema kuwa ili kuondoa changamoto zote wanazokutana nazo wakulima hao ni lazima watengeneze vikundi vya wakulima wa mwani ili kutengeneza umoja utakaosaidia kupata soko la uhakika na kuongeza tija kwa wakulima hao.