Wananchi Msimbati wafurahia ujenzi wa kituo cha afya
10 September 2024, 08:18 am
Ujenzi wa kituo cha afya katika kijiji cha Mtandi kata ya Msimbati ni katika kutekeleza maagizo yaliyotolewa na naibu Waziri mkuu na waziri wa nishati DK Dotto Biteko alipofanya ziara katika eneo na kutoa maagizo ya kuwajengea kituo cha afya,kituo cha Polisi ,taa za Barabarani kupitia fedha za mrejesho wa jamii (CSR) zinazptokana na uzalishaji wa Gesi Asilia katika eneo hilo.
Na Musa Mtepa
Wananchi wa kata ya Msimbati wameishukuru serikali kwa kitendo cha kuwajengea kituo cha afya kitakachosaidia kupunguza baadhi ya gharama walizokuwa wanazitumia kuzifuata huduma za afya umbali umrefu.
Wananchi hao wamesema kuwa huduma za afya za uhakika wanazipata katika hospitali ya mkoa ya Ligula ambayo ipo umbali mrefu kutoka katika Kijiji hicho.
Naye Mbunge wa jimbo la Mtwara vijijini Mh Shemsia Mtamba ameishukuru serikali kwa kusikiliza kilio cha wakazi wa kata ya Msimbati kwa kuwajengea kituo hicho afya na kumuomba naibu Waziri wa nishati Judith Kapinga kupeleka shukrani hizo kwa Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Daktari Samia Suluhu Hassani.
Akizungumza na Wananchi wa Msimbati Naibu Waziri wa Nishati amesema kuwa hadi kufikia September 30,2024 kituo hicho kitakuwa kimekamilika na tayari kwa kuanza kutoa huduma.