Wananchi mikoa ya kusini kunufaika na mikopo ya kilimo
10 July 2023, 16:20 pm
Wananchi wa mikoa ya kusini Lindi, Mtwara na Ruvuma wametakiwa kuchangamkia fursa ya uwepo wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Kanda ya Kusini katika kupata uelewa na utaratibu wa kupata mikopo ili kupata vifaa vya kisasa vitakavyowezesha kuleta tija kwenye kilimo.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa Benki hiyo Kanda ya Kusini Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kasim Majaliwa amesema kuwa wakulima hawana budi kwenda kupata mikopo itakayowezesha katika shughuli mbalimbali za kilimo ili iweze kuleta tija.
Aidha Waziri Mkuu amewataka wanufaika wa mikopo kufanya matumizi sahihi ya fedha wanazokopeshwa ili kuendeleza miradi waliyoombea.
Akitoa salamu kwa Waziri mkuu , Mkuu wa Mkoa Mtwara Kanali Ahmed Abasi amesema kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan, mkoa umepokea zaidi shilingi bilioni 619.6 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati .
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Mtwara Mjini Hassani Mtenga ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kutoa huduma karibu na wananchi huku akimwomba Waziri Mkuu kuangalia namna ya kutumia bandari ya Mtwara katika usafirishaji wa korosho.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atakuwepo mkoani Mtwara hadi Julai 14, 2023 katika ziara ya kikazi akikagua na kujionea miradi mbalimbali inayotekelezwa katika halmashauri zote zilizopo mkoani Mtwara ambapo hii leo atakuwepo halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani.