Jamii FM
Jamii FM
10/03/2026, 10:02

Mtoto Yasri Hamisi (14) wa kijiji cha Ndumbwe, Mtwara, anahofiwa kufariki baada ya kutumbukia mtoni alipoteleza akijaribu kugusa maji wakati akiwa na wenzake. Wananchi na vikosi vya uokoaji wanaendelea na juhudi za kumtafuta
Na Musa Mtepa
Mtoto Yasri Hamisi, mwenye umri wa miaka 14, mkazi wa kijiji cha Ndumbwe, wilaya na mkoa wa Mtwara, anahofiwa kupoteza maisha baada ya kutumbukia katika mto unaopita kijijini hapo ukitokea Bwawa la Kitere kuelekea Bahari ya Hindi upande wa Ndumbwe.
Inaelezwa kuwa Yasri aliambatana na wenzake watatu mnamo March 7, 2026 kwenda katika mto huo kwa ajili ya kufanya shughuli za uvuvi. Hata hivyo, walipofika mtoni walibadili maamuzi ya kuvua samaki na kuamua kuoga. Mmoja wao aliwaonya wenzake kuwa maji yalikuwa mengi na yana kasi hivyo yeye hangeweza kuoga.
Inadaiwa kuwa Yasri alipokuwa akijaribu kugusa maji kwa mguu ndipo alipoteleza na kutumbukia mtoni na kuzama.
Wakizungumzia tukio hilo jana, March 9, 2026, wakazi wa kijiji cha Ndumbwe wamesema wanaendelea na juhudi za kumtafuta kijana huyo kwa kufuata mwelekeo wa maji yanakoelekea kuchanganyika na maji ya Bahari ya Hindi.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa kijiji cha Ndumbwe Ali Mshamu amekiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa baada ya kupata taarifa alitoa taarifa kwa wananchi wa kijiji kizima ili kuanza jitihada za kumtafuta kijana huyo. Hata hivyo hadi kufikia jana, March 9, 2026, bado hawajafanikiwa kumpata.

Akizungumzia tukio hilo, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Ambrosi Ndunguru amesema kuwa baada ya kupokea taarifa ya tukio hilo, timu ya uokoaji ya jeshi hilo ilifika katika kijiji cha Ndumbwe na kuanza operesheni ya kumtafuta kijana huyo, lakini hadi sasa hawajafanikiwa kumpata baada ya juhudi za siku mbili huku akisema kuwa zoezi la utafutaji litaendelea kwa siku ya tatu.
Aidha, Mrakibu Ndunguru ametoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuepuka kusogelea mto huo kwa shughuli za uvuvi au kilimo kwa sasa, kutokana na kufurika kwa maji yenye kasi yanayotoka katika Bwawa la Kitere pamoja na vijiji vya pembezoni.
