Jamii FM

Zaidi ya tani 9,000 za salfa zawasili bandari ya Mtwara

10 March 2025, 18:46 pm

Frances Alfred Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya korosho Tanzania (CBT)akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili kwa meli iliyobeba pembejeo ya salfa

Hii ni meli ya kwanza kati ya meli nne zinazotarajia kubeba tani 40,000 za pembejeo  ya zao la korosho kwa msimu wa mwaka 2025/2026 ambapo kwa mujibu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho wakulima wanahitaji tani 40’000 ili kufanikisha uzalishaji unaokusudiwa .

Na Musa Mtepa

Zaidi ya tani 9,000 kati ya tani 40,000 za salfa zinazotarajiwa kupokelewa kwa mwaka wa kilimo wa zao la korosho 2025/26 zimepokelewa katika bandari ya Mtwara, ikiwa ni maandalizi ya msimu mpya wa kilimo wa zao la korosho.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mapokezi ya meli iliyobeba salfa hizo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Frances Alfred, amesema kwamba Bodi imepanga kuleta salfa zaidi ya tani 40,000 kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wakulima wa zao la korosho nchini. Hivyo, ujio wa meli iliyobeba tani 9,202 za salfa ni sehemu ya meli nne zinazotarajia kuleta tani 40,000 za pembejeo kwa ajili ya msimu wa kilimo wa korosho 2025/2026.

Sauti ya 1 Frances Alfred Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya korosho Tanzania (CBT)

Aidha, Mkurugenzi Mkuu metumia fursa hiyo kuwasihi wakulima wa zao la korosho kuhakikisha wanaenda kuhuisha taarifa zao kwa maafisa ugani ili waweze kufaidika na ruzuku ya pembejeo zinazotolewa na serikali.

Sauti ya 2 Frances Alfred Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya korosho Tanzania (CBT)

Kwa upande mwingine, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Ferdinand Nyathi, amesema kuwa Bandari hiyo inaendelea kutengeneza historia katika kuhudumia meli zinazobeba viuatilifu vya zao la korosho huku akiongeza kuwa Bandari  imejizatiti kuhakikisha usalama wa pembejeo hizo na maandalizi mengine muhimu kabla ya kufikishwa kwa wakulima.

Sauti ya Ferdinand Nyathi Meneja wa Bandari ya Mtwara

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Michael Mtenjele, ambaye amezungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, amesisitiza kuwa maafisa wanaohudumia pembejeo hizo wanatakiwa kufuata taratibu ili kuhakikisha  pembejeo zinawafikia wakulima kama ilivyokusudiwa.

Sauti ya Kanali Michael Mtenjele Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba.

Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara, Juma Namkoveka, amesisitiza kwamba Bodi ya Korosho na wadau wengine wanapaswa kuhakikisha pembejeo hizo zinawafikia wakulima kwa wakati na ilivyokusudiwa ili kutimiza lengo la kuongeza uzalishaji wa zao la korosho nchini.

Sauti ya Juma Namkoveka katibu wa siasa na uenezi CCM mkoa wa Mtwara

Katika mwaka wa kilimo wa 2025/26, serikali ya Tanzania imeongeza juhudi katika kuboresha uzalishaji wa zao la korosho, na hatua hii ya kupokea pembejeo mapema ni moja ya mikakati ya kuhakikisha kuwa wakulima wanapata msaada wa kutosha kwa ajili ya mafanikio ya kilimo cha korosho.