Jamii FM
Jamii FM
9 November 2025, 12:14 pm

Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imeruhusu usafirishaji wa korosho saa 24 kwa mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara ili kuharakisha uondoaji wa mizigo na kuongeza ufanisi wa Bandari ya Mtwara. Katika mnada wa kwanza, TANECU iliuza tani 26,000 kwa bei ya juu ya Sh. 3,520 kwa kilo
Na Musa Mtepa
Tandahimba-Mtwara, Novemba 8, 2025 Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imeruhusu magari yote yanayosafirisha korosho kutoka mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara kufanya usafirishaji wa korosho masaa 24, usiku na mchana.
Hata hivyo, mikoa mingine itaendelea kusafirisha korosho kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni kama kawaida.
Hatua hiyo inalenga kuharakisha uondoaji wa mizigo kwenye maghala makuu ili kutoa nafasi kwa korosho nyingine za wakulima kuingia ghalani kwa ajili ya minada inayofuata.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi rasmi wa msimu wa minada wilayani Tandahimba, Mkurugenzi Mkuu wa CBT, Ndugu Frances Alfred, amesema kuwa ruhusa hiyo inahusisha mikoa inayosafirisha korosho kupitia Bandari ya Mtwara au maghala makuu yaliyopo mjini Mtwara.
Aidha, Ndugu Frances amesema kuwa sababu kubwa ya kutoa ruhusa hiyo ni kuhakikisha korosho zinatoka kwa haraka katika maghala makuu ili korosho nyingine za wakulima ziweze kuingizwa kwa ajili ya minada inayofuata.
Ameeleza kuwa hatua hiyo pia inalenga kuongeza mzunguko wa malori, kuboresha ufanisi wa Bandari ya Mtwara katika kurahisisha usafirishaji wa korosho nje ya nchi, pamoja na kuwavutia wanunuzi zaidi kushiriki katika minada mingine ijayo ya zao hilo.

Novemba 8, 2025, mnada wa kwanza wa zao la korosho umefanyika katika wilaya ya Tandahimba, ambapo Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU Ltd) kimefanikiwa kuuza korosho tani 26,000 na kilo 254.
Bei ya juu katika mnada huo ilikuwa shilingi 3,520 kwa kilo, huku bei ya chini ikiwa shilingi 2,550 kwa kilo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa TANECU, Ndugu Karim Chipola, katika jumla hiyo ya korosho zilizouzwa, Tandahimba imechangia tani 18,102, huku Newala ikichangia tani 8,152.