Jamii FM

Wakulima waomba bei bora zaidi ya korosho

9 November 2025, 09:31 am

Viongozi wa Bodi ya Korosho,TANECU na Serikali wakiwa katika uzinduzi wa rasmi wa mnada wa Korosho msimu wa 2025/2026 katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Tandahimba (Picha na Musa Mtepa)

Wakulima wa korosho wilayani Tandahimba wamepokea kwa mitazamo tofauti bei ya zao hilo katika mnada wa kwanza wa msimu 2025/2026, ambapo kilo moja imenunuliwa kwa bei ya juu ya shilingi 3,520 na ya chini shilingi 2,550, huku wakitaka wanunuzi kuongeza bei ili kuendana na gharama za uzalishaji

Na Musa Mtepa

Wakulima wa zao la korosho wamepokea kwa mitazamo tofauti bei ya zao hilo kupitia mnada wa kwanza uliofanyika tarehe 8 Novemba 2025, wilayani Tandahimba, mkoani Mtwara. Katika mnada huo, bei ya juu kwa kilo moja ya korosho imeuzwa kwa shilingi 3,520 na kwa shilingi 2,550 kwa bei ya chini.

Mnada huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba, kupitia Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU), ambapo zaidi ya tani 26,000 za korosho zimeuzwa.

Wakulima wameishukuru serikali na vyama vya ushirika kwa kufanikisha mnada huo, huku wakitoa wito kwa wanunuzi kuongeza bei ya korosho ili iendane na gharama kubwa za uzalishaji wa zao hilo.

Sauti ya wakulima wa korosho wilayani Tandahimba
Wakulima wa zao Korosho wakifuatilia mwenendo wa soko la korosho katika mnada wa kwanza wa uzinduzi wa msimu wa korosho nchini uliofanyika wilayani Tandahimba(Picha na Musa Mtepa)

Bi. Tatu Mahupa mkulima wa korosho amefurahi kufanyika kwa mnada huo huku akiwataka wakulima kutumia vizuri fedha watakazopata kutokana na mauzo ya korosho, kwa kuweka bajeti nzuri ya matumizi na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima, ili ziweze kusaidia katika mahitaji muhimu ya familia ikiwemo elimu ya watoto.

Sauti ya Tatu Mahupa, mkulima wa korosho, Mchichira.

Akiongoza mauzo katika mnada huo, Mwenyekiti wa TANECU Ltd, Karim Chipola, amewapongeza wakulima kwa mwitikio wao mkubwa. Amesema kati ya tani 26,000 na kilo 254 zilizouzwa, Tandahimba imechangia tani 18,102 na Newala tani 8,152, zikiuzwa kwa bei ya juu ya shilingi 3,520 na bei ya chini shilingi 2,550 kwa kilo.

Sauti ya Karim Chipola, Mwenyekiti wa TANECU.
Mwenyekiti wa TANECU,Ltd akizungumza na wakulima waliojitokeza kwenye mnada huo(Picha na Musa Mtepa)

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Bw. Godfrey Marekano, amesema matarajio yao ni kuona idadi ya wanunuzi inaongezeka katika minada inayofuata ili kuongeza ushindani na hatimaye kuinua bei ya korosho kwa manufaa ya wakulima.

Sauti ya Godfrey Marekano, Afisa Mtendaji Mkuu wa TMX.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Ndugu Frances Alfred, amesema mnada huo ni wa kwanza kitaifa kwa msimu wa 2025/2026, na ndio unaoashiria mwenendo wa soko la kimataifa la korosho kwa mwaka huu.

Sauti ya – Frances Alfred, Mkurugenzi Mkuu wa CBT