Jamii FM

TARI yaeleza mbinu za kudhibiti ubwili unga kwenye mikorosho

8 June 2025, 19:38 pm

Stanlaus Lilai mtaalum wa uthibiti wa visumbufu TARI Naliendele akionesha mfano wa ugonjwa wa ubwili unga unavyoathiri kwenye mikorosho (Picha na Musa Mtepa)

Stanslaus Lilai alikuwa anatoa Elimu hiyo kwenye mafunzo ya maafisa ugani wa halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani ikiwa njia mojawapo ya kufika elimu hiyo kwa wakulima kupitia maafisa hao

Na Musa Mtepa

Wakulima wa zao la korosho nchini wameaswa kutambua na kuchukua hatua za haraka dhidi ya ugonjwa wa Ubwili unga, ambao umeendelea kuleta athari kubwa katika uzalishaji wa zao hilo.

Hayo yamesemwa na  Stanslaus Lilai, mtafiti na mtaalamu wa uthibiti wa visumbufu vya zao la korosho kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) – Naliendele,ambapo amesema kuwa ugonjwa wa Ubwili unga hushambulia karibu sehemu zote muhimu za uzalishaji wa korosho, ikiwa ni pamoja na majani machanga, maua na korosho changa (tegu).

Sauti ya 1 Stanlaus Lilai mtaalum wa uthibiti wa visumbufu TARI Naliendele

Kwa mujibu wa Lilai, amesema kabla ya mkulima hajaanza zoezi la upuliziaji wa viuatilifu, ni muhimu kutambua kwa usahihi dalili za ugonjwa huo ambazo huonekana zaidi kwenye majani machanga, maua na korosho changa, ambapo mmea huonyesha mabadiliko kama vumbi jeupe, kudhoofika kwa ukuaji na hatimaye kuanguka kwa maua au matunda changa.

Sauti ya 2 Stanlaus Lilai mtaalum wa uthibiti wa visumbufu TARI Naliendele

Kuhusu mbinu za kudhibiti ugonjwa huo, Lilai ameeleza kuwa kuna njia nyingi zinazoweza kusaidia, ikiwemo kufanya usafi wa mikorosho (kupunguza mazalia ya visumbufu),kutumia mbegu bora zenye ukinzani dhidi ya magonjwa pamoja na upuliziaji wa viuatilifu vyenye viambata amilifu vinavyoweza kudhibiti Ubwili unga.

Sauti ya 1 Stanlaus Lilai mtaalum wa uthibiti wa visumbufu TARI Naliendele

TARI Naliendele imeendelea kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu mbinu bora za kukabiliana na magonjwa ya mikorosho ili kuongeza tija na ubora wa mazao ya korosho nchini ikiwa katika kutimiza lengo la kufikia tani 700,000 ifikapo mwaka 2026.

Baadhi ya maafisa ugani wakiwa katika mafunzo ya matumizi salama na sahihi ya viuatilifu vya zao la korosho (Picha na Musa Mtepa)