Meli Kubwa yatia Nanga Bandari ya Mtwara kubeba Makaa ya Mawe
8 January 2022, 14:05 pm
“Meli kubwa ya Star fighter ambayo itaondoka na tani elfu 59 za makaa yam awe, Sisi tumefurahi sana ujio wake, na uzito unaoondoka hapa kwa upande ule wa gati ya zamani tusingeweza kuipaki kwa tani elfu 59, uboreshaji na ujenzi wa Bandari mpya ndio umesababisha meli hii kupaki hapa, sisi kama bandari Mtwara tutahakikisha wanakusini tunawaletea maendeleo kupitia Bandari”
Abdillah Salim – Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara
Na Gregory Millanzi, Mtwara
Meli kubwa yenye urefu wa Mita 200 imetia nanga kwenye gati mpya ya Bandari ya Mtwara kwa ajili ya kubeba Tani elfu 59 za Makaa ya Mawe ambayo yanatarajiwa kusafirishwa kupelekwa nchini India, meli hiyo imetokea Pakistani.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya Meli hiyo jana Januari 8,2022, Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Bandari Mtwara Abdillah Salim amesema, meli hiyo ni meli kubwa sana kuwahi kutia nanga kwenye bandari hiyo na kutokana na uwepo wa gati nkubwa mpya iliyojenjwa na Serikali imesaidia kuweza kuhimili meli hiyo kutokana na uzito wa mzigo ambao utabeba wa Tani elfu 59 ambayo kwa Gati la zamani isingeweza kuhimili.
Salim amesema, uwepo wa Meli hiyo ni moja ya maendeleo ya Bandari na Mkoa kwa ujumla na utaratibu wa kupakia Makaa ya mawe utachukua siku saba ili kuweza kupakia tani elfu 59 kwenye meli hiyo.
“Meli kubwa ya star fighter ambayo itaondoka na tani elfu 59 za makaa yam awe, Sisi tumefurahi sana ujio wake, na uzito unaoondoka hapa kwa upande ule wa gati ya zamani tusingeweza kuipaki kwa tani elfu 59, uboreshaji na ujenzi wa Bandari mpya ndio umesababisha meli hii kupaki hapa, sisi kama bandari Mtwara tutahakikisha wanakusini tunawaletea maendeleo kupitia Bandari” amesema Abdillah Salim, kaimu Meneja wa bandari ya Mtwara.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya alisema ujio wa meli hiyo ni faraja kwa wananchi wa Mtwara kwani uwepo wa Bandari hii hasa gati jipya unaweza kuchangia kukuza uchumi wa Mkoa wa Mtwara na Tanzania kwa ujumla, pia ni Fursa ya Wananchi kujipatia kazi kwa ujio wa meli hizi zinazokuja.
“Ujio wa Meli hii ni moja ya maendeleo makubwa kwa wananchi wa Mtwara na Tanzania kwa ujumla, Pia ni pongezi kwa Serikali kwa kujenga gati jipya ambalo limewezesha meli hii kutia nanga, Nimefarijika sana ujio wa meli hii na niwapongezi Bandari na kampuni ya Ruvuma Mining kwa kuleta Meli hii kubwa, na bandari hii inaweza kutumika kwa shighuli mbalimbali tofauti na zao la Korosho” Amesema Dunstan Kyobya, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara.
Mkurugenzi wa Huduma za Meli na utekelezaji wa Shughuli za Kibandari Mamlaka ya Bandari Tanzania Kapteni Mwingamno alisema, Hii ndio shehens kubwa sana kuwahi kuchukuliwa ya makaa yam awe kwenye bandari ya Mtwara kwa wakati mmoja, kwa sasa upakiaji utachukua siku saba kutokana na vifaa vilivyopo kwa sasa, lakini serikali ipo kwenye mpango Mkubwa wa kuleta vifaa vya kupakilia ambavyo tayari vimeshaagizwa na vunatarajiwa kufungwa kwenye gati jipya na kwa meli kama hii kwa vifaa vitakavyofungwa itachukua siku tatu kupakia ili kurahisisha kazi Babdarini.
Hii ndio meli ya kwanzakubwa kutia nanga kwenye Gati Mpya ya Bandari ya Mtwara ambayo imejengwa na Serikali kwa gharama ya Shilingi Bilioni 157.8.