Jamii FM

TADIO yawanoa wanahabari Jamii FM Mtwara

7 January 2025, 12:15 pm

Mhariri kutoka Radio Tadio Hilali Ruhundwa akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari wa kituo cha redio cha Jamii FM, kilichopo Mtwara (Picha na Mohamed Masanga)

Mafunzo haya yametolewa na jukwaa la redio za kijamii Tanzania (radio tadio) kwa lengo la kuwakumbusha waandishi wa habari na watangazaji kufanya kazi kwa kufuata madili ya uandishi wa habari katika kazi zao hasa wakati wa uchaguzi mkuu.

Na Musa Mtepa

Jukwaa linalounganisha redio za kijamii Tanzania (Radio Tadio) limeendelea kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari wanachama, yakilenga kuimarisha misingi ya uandishi wa habari, hasa kwa kuzingatia namna ya kuandika na kuripoti habari za uchaguzi pasipo kuleta taharuki kwenye jamii.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo yaliyofanyika Januari 6, 2025 kwa waandishi wa habari kutoka Jamii FM redio, Hilali Ruhundwa, Mhariri wa radiotadio.co.tz, amesema kuwa mafunzo hayo yana lengo la kuwafundisha waandishi wa habari kuhusu maadili ya uandishi na jinsi ya kuandika habari zinazowaunganisha watu, wagombea na kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki.

Ruhundwa amesisitiza kuwa ni muhimu waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi kwa umma kupitia vyombo vya habari ili wananchi wapate taarifa sahihi na kufanya maamuzi sahihi katika uchaguzi.

Sauti ya 1 Hilali Ruhundwa – Mhariri, Radio Tadio

Hilali Ruhundwa ameongeza kuwa mafunzo haya ni muhimu kwa waandishi wa habari wa vyombo vya jamii, kwani yatasaidia kuelewa misingi ya kuandika habari kwa usawa, hivyo kuepuka kuleta mivutano au taharuki wakati wa kuripoti matukio ya uchaguzi. Pia amewahimiza washiriki kuyazingatia mafunzo waliyopata kwani yatawasaidia katika kazi zao za kila siku, hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Sauti ya 2 Hilali Ruhundwa – Mhariri, Radio Tadio

Gregory Milanzi, mmoja wa waandishi wa habari kutoka Jamii FM Redio, amesema kuwa kupitia mafunzo hayo ameongeza ufahamu wake kuhusu jinsi ya kuandika na kutangaza habari kwa usawa na ukweli. Milanzi ameeleza kuwa mafunzo hayo yatamsaidia pia kuzingatia uhalisia wa maeneo wanayofanyia kazi, jambo litakalosaidia kuleta usawa katika ripoti zinazowahusu wananchi.

Sauti ya Gregory Milanzi – Mwandishi wa habari, Jamii fm redio

Kwa upande mwingine, Mwanaidi Kopakopa, mtangazaji wa Jamii FM redio, ametoa shukrani kwa Jukwaa la Redio za Kijamii Tanzania kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu pamoja na kusema  kuwa mafunzo haya yatawabadilisha na kuwafanya waandishi wa habari kuwa bora zaidi katika uandishi wao, hasa kwa kuzingatia maadili ya kazi yao wakati nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Sauti ya Mwanaidi Kopakopa – mtangazaji, Jamii fm redio

Hii inaonyesha umuhimu wa mafunzo hayo katika kuhakikisha waandishi wa habari wanazingatia maadili ya uandishi na kuchangia katika uchaguzi huru na haki kwa kutoa taarifa sahihi kwa jamii. Jukwaa la Redio za Kijamii Tanzania linaendelea kuwa daraja muhimu katika kuhakikisha waandishi wanazingatia uandishi wa habari unaozingatia usawa, ukweli, na umoja wa jamii.