Jamii FM
Jamii FM
06/03/2026, 09:03

Wananchi katika vijiji vya Lindi na Mtwara walalamikia kuchelewa kulipwa fidia ya mazao yaliyoharibiwa wakati wa utafiti wa mafuta na gesi, huku TPDC ikisema tathmini imefikia asilimia 51 na malipo yanatarajiwa kuanza
Na Musa Mtepa
Wananchi wanaoishi katika vijiji vilivyopitiwa na mradi wa utafiti wa gesi na mafuta katika wilaya za Lindi na Mtwara wamelalamikia kuchelewa kulipwa fidia ya mazao yao yaliyoharibiwa wakati wa kuweka njia za kupita mitambo ya utafiti.
Wananchi hao wamesema kuwa utafiti wa mafuta na gesi ni jambo muhimu kwa uchumi na maendeleo ya taifa, lakini wanashangazwa na kuchukua muda mrefu kulipwa fidia ya mazao yao yaliyoondolewa wakati wa shughuli za utafiti huo.
Akizungumza Febraury 28,2026 Hamza Karimu Mrope, mwenyekiti wa kitongoji cha Likuluwilo katika kijiji cha Hiari, wilayani Mtwara, amesema jamii inashukuru kwa uwepo wa utafiti huo lakini wananchi wanashangaa kwa nini fidia ya mazao yao yaliyoondolewa wakati wa utafiti imechukua muda mrefu kulipwa.

Kwa upande wake, Mohamedi Mbaki ambaye ni Diwani wa Kata ya Mayanga amesema ni kweli kuwa hadi sasa wananchi hawajalipwa fidia hiyo. Amesema ni muhimu kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuhakikisha fedha za fidia zinalipwa kwa wakati ili wananchi wanufaike na mazao yao yaliyotolewa wakati wa utafiti wa mafuta na gesi katika mashamba yao.
Sauti ya Mohamedi Mbaki Diwani kata ya Mayanga
Akitoa ufafanuzi kuhusu malalamiko hayo, Mjiolojia na Meneja wa Mradi wa Utafiti wa Mafuta na Gesi Asilia kupitia kitalu cha Lindi/Mtwara, Dkt Shaidu Nuru, amesema zoezi la tathmini ya fidia katika mradi huo wenye ukubwa wa kilometa za mraba 736.3 limekamilika kwa asilimia 51, na hatua iliyobaki ni malipo ya fidia.
Amesema utaratibu uliopo sasa ni kuandaa vitabu vitakavyowasilishwa kwa maafisa mbalimbali kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa malipo, na zoezi hilo tayari limekamilika.
Aidha, Dkt Nuru amesema jumla ya shilingi milioni 477.9 zimeidhinishwa na Mthamini Mkuu kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi 2,571 walioathiriwa na mradi huo. Ameongeza kuwa awali walikuwa wamepanga ifikapo mwezi Februari 2026 wawe tayari wameanza kulipa fidia hiyo.
