Jamii FM

Jamii FM yatoa tuzo kwa wasikilizaji bora wa mwaka 2025

5 January 2026, 16:00 pm

Mkurugenzi wa jamii fm radio Ndug Swalla Saidi Swalla akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa tuzo,wasikilizaji wa vipindi na wafanyakazi wa kituo hicho(Picha na Mohamedi Masanga)

Jamii FM Redio imetangaza wasikilizaji na wachangiaji bora wa vipindi vyake kwa mwaka 2025. Washindi walichaguliwa na wasikilizaji kupitia SMS na kukabidhiwa tuzo katika hafla iliyofanyika katika studio za kituo hicho

Na Musa Mtepa

Jamii FM Redio imetangaza wasikilizaji na wachangiaji bora wa vipindi vyake kwa mwaka 2025, katika hafla iliyofanyika Jumatano Desemba 31, 2025, katika kituo cha kurushia matangazo cha Jamii FM Redio kilichopo Mtwara.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mkurugenzi wa Jamii FM Redio, Bw. Swallah Said Swallah, alimtangaza Ndg. Mambo Katani, mtoto wa Fatu Mohamedi Kumbuko kutoka kijiji cha Rondo Ntene, Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi, kuwa msikilizaji na mchangiaji bora wa kiume. Aidha, Bi. Amina Mkanjima, binti wa Mkanjima maarufu kama Mama wa Yanga (Mama Bakari Kitemwe) kutoka Manispaa ya Mtwara Mikindani, alitangazwa kuwa msikilizaji na mchangiaji bora wa kike.

Sauti ya Swallah Said Swallah, Mkurugenzi wa Jamii FM Redio

Bw. Swallah amesema kuwa utaratibu wa kutambua na kuwazawadia wasikilizaji na wachangiaji bora ulianza rasmi mwaka 2024 na utaendelea kila mwaka, huku kituo kikiendelea kuboresha mifumo ya upatikanaji wa washindi pamoja na thamani ya zawadi zitakazotolewa kadri miaka inavyoendelea.

Sauti ya Swallah Said Swallah, Mkurugenzi wa Jamii FM Redio

Akizungumzia malengo ya kituo hicho, Bw. Swallah ameeleza kuwa kuanzishwa kwa Jamii FM chini ya MTUKWAO Community Media kunalenga kuibua, kuchakata na kurusha taarifa za kijamii ambazo mara nyingi hazipewi nafasi katika vyombo vingine vya habari na kubainisha kuwa lengo la MTUKWAO COMMUNITY MEDIA kuwa na kituo hicho cha redio na televisheni ya kijamii (Community Television – CTV).

Sauti ya Swallah Said Swallah, Mkurugenzi wa Jamii FM Redio

Uchaguzi wa washindi ulifanyika kwa kuwashirikisha wasikilizaji wenyewe kupitia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS), ambapo walipiga kura kumchagua msikilizaji na mchangiaji bora wa kike na wa kiume.

Nao baadhi ya washiriki waliofanikiwa kufika hatua ya washiriki 15 bora wameipongeza Jamii FM Redio kwa kuandaa tuzo hizo, wakieleza kuwa hatua hiyo imeongeza hamasa ya ushiriki wa vipindi na kuwapongeza washindi waliopata tuzo kwa mwaka 2025.

Sauti ya washiriki wa tuzo za uchangiaji na usikilizaji bora

Kwa upande wao, Bi. Amina Mkanjima na Ndg. Mambo Katani, washindi wa tuzo za msikilizaji na mchangiaji bora kwa mwaka 2025, wameishukuru Jamii FM Redio pamoja na wasikilizaji wote kwa kuwaamini na kuwachagua. Pia wametoa wito kwa wasikilizaji wengine kuendelea kufuatilia na kuchangia vipindi vya redio hiyo kwa kuzingatia maadili, utaratibu na kuheshimu haki za wengine bila kumdhuru mtu yeyote.

Sauti ya washindi wa tuzo

Naye Meneja wa Jamii FM Redio, Bw. Amua Rushita, amewashukuru wasikilizaji wa Jamii FM Redio kwa kuendelea kuisikiliza redio hiyo kwa mwaka 2025, huku akiukaribisha mwaka 2026 kwa kauli mbiu isemayo “Mtaa kwa Mtaa.”

Jumla ya washiriki kumi na tano (15) walichaguliwa kufikia hatua ya mwisho ya mashindano, ambapo wawili kati yao waliibuka washindi.

Washindi wamekabidhiwa zawadi ya redio aina ya Subwoofer yenye thamani ya shilingi laki moja na elfu hamsini (Tshs 150,000/=) kila mmoja.