Jamii FM
Jamii FM
4 January 2026, 12:45 pm

Wananchi wa Kilambo na maeneo ya mpakani na Msumbiji wanaiomba Serikali kurejesha kivuko cha MV Kilambo kilichosimama kufanya kazi, Serikali imesema matengenezo yanaendelea
Na Musa Mtepa
Wananchi na watumiaji wa kivuko cha Kilambo kinachounganisha Tanzania na nchi jirani ya Msumbiji wamehoji ni lini kitarejea na kuiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kurejesha huduma ya feri ya MV Kilambo, ili kuondoa usumbufu na gharama kubwa wanazokumbana nazo kwa sasa.
Wakizungumza na waandishi wa habari, wakazi wa eneo hilo wamesema hali ya usafiri si ya kuridhisha, kwani wanalazimika kutumia viboti vidogo kuvuka mpaka wa maji, ambavyo si salama na vina gharama kubwa ikilinganishwa na huduma ya awali ya feri.
Ahamadi Hassani na Ahamadi Fuka, wakazi wa Kijiji cha Kilambo katika Halmashauri ya Mtwara Vijijini, wanasema kutokuwepo kwa feri hiyo kunawalazimu kutumia vyombo vya majini visivyo salama, hali inayohatarisha maisha yao na kuongeza gharama za usafiri.
Kwa upande wake, Rajabu Athumani Salumu, dereva wa bodaboda kutoka kijiji hicho, amesema ukosefu wa chombo cha uhakika cha usafiri umesababisha mlundikano wa abiria na mizigo, huku baadhi ya wasafiri wakilazimika kulala eneo hilo kwa zaidi ya siku tatu wakisubiri usafiri.

Naye Fatuma Bakari, mkazi wa Kijiji cha Singa kilichopo nchini Msumbiji, amesema ucheleweshaji unaotokana na kutokuwepo kwa kivuko hicho ni changamoto kubwa kwa wakazi wa pande zote mbili za mpaka, hasa kwa shughuli za kibiashara na kijamii.
Akitoa ufafanuzi kwa njia ya simu, Meneja wa Vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini, Abdulrahman Amir, amesema feri ya MV Kilambo ilipelekwa kufanyiwa matengenezo, lakini baada ya kukamilika ilirejeshwa Mtwara Mjini kutokana na changamoto za kiusalama na miundombinu katika eneo la Kilambo–Namoto kwa kipindi hicho.

Ameongeza kuwa kutokana na kivuko hicho kukaa muda mrefu bila kufanya kazi, kinahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa pamoja na kuboreshwa kwa miundombinu ya kuegeshea feri katika eneo la Kilambo.
Aidha, amesema TEMESA inatarajia kuingia mkataba kwa ajili ya matengenezo hayo makubwa, huku matarajio ya kurejea kwa huduma ya kivuko cha MV Kilambo kwa wananchi yakiwa ni kuanzia mwishoni mwa mwezi Februari mwaka 2026.