TANECU kuwakomboa wakulima wa korosho Mtwara
3 October 2024, 12:48 pm
Kiwanda hiki kinakadiriwa kuwa na thamani ya shilingi bilioni 3.4 huku kikitarajiwa kubangua tani 3,500 za korosho kwa mwaka.
Na Musa Mtepa
Wakulima wa korosho katika wilaya za Tandahimba na Newala mkoani Mtwara wameonesha furaha yao kuhusu ujenzi wa kiwanda cha kubangua korosho kilichojengwa na Chama Kikuu cha Ushirika TANECU LTD katika kijiji cha Mmovo.
Wakulima hawa wamesema uwepo wa kiwanda hicho unawapa matumaini makubwa na usalama katika kutimiza malengo yao ya kiuchumi kupitia zao la korosho.
Halima Salumu Mtale, mkazi wa Newala na msimamizi wa shughuli za ubanguaji, amesema kiwanda kitawasaidia akina mama kiuchumi kwa kuwapa uwezo wa kujikimu na kugharamia mahitaji kama vile kulipa kodi na kusomesha watoto.
Mwenyekiti wa TANECU, Karim Chipola, ameishukuru serikali kwa kusaidia ujenzi wa kiwanda hiki na kuwashauri wakulima wa Tandahimba na Newala kuwa na matumaini, hasa baada ya changamoto ya miaka mitatu iliyopita ya kupungua kwa bei ya korosho sokoni.
Aidha, Chipola amesema wamejipanga kuhakikisha wanakuwa na masoko ya uhakika kwa korosho karanga, ndani na nje ya nchi.
Chama Kikuu cha Ushirika TANECU LTD kinahudumia wakulima wa wilaya hizi na kina malengo ya kujenga viwanda 10 kwa kila wilaya, ili kuboresha thamani ya zao la korosho na kuwaa na manufaa kwa wakulima.