Jamii FM
Jamii FM
3 January 2026, 18:18 pm

Wakulima wa korosho Nanyamba wamelalamikia tofauti kubwa ya bei ukilinganisha na Tandahimba, hali inayowalazimisha kuhamishia mazao yao Tandahimba
Na Musa Mtepa
Wakulima wa zao la korosho katika Halmashauri ya Mji Nanyamba wamehoji tofauti ya bei ya korosho inayojitokeza sokoni kati ya halmashauri hiyo na Wilaya ya Tandahimba, hali inayowalazimu baadhi yao kupeleka mazao yao Tandahimba ili kupata bei ya juu zaidi.
Wakizungumza na waandishi wa habari, wakulima hao wamesema kuwa kwa takribani miaka kumi sasa bei ya korosho imekuwa hairidhishi, huku tofauti ya bei kati ya Nanyamba na Tandahimba ikiendelea kuwa kubwa.
Wamesema kuwa licha ya madai ya kuwepo kwa unyevu kwenye korosho zinazouzwa Nanyamba, korosho hizo hizo zikipelekwa Tandahimba hununuliwa kwa bei ya juu zaidi.
Wakizungumzia sababu za utofauti wa bei ndani ya mnada mmoja, wakulima hao wamesema kuwa mfumo wa ununuzi wa korosho kwa njia ya loti unaochangia tofauti ya bei kati ya Halmashauri ya Nanyamba na maeneo mengine ya Mtwara, Masasi pamoja na Nanyumbu.
Jamali Nalyogo, mkulima kutoka Mtimbwilimbwi, pamoja na Issa Kamkunje wa kijiji cha Njengwa wamesema hali hiyo imekuwa ikiwasababishia maumivu ya moyo, huku wakilaumu wawakilishi (Wabunge) na viongozi wanaosimamia zao la korosho katika Halmashauri ya Nanyamba,Mtwara,Masasi na Nanyumbu kutowatendea haki.

Kwa upande wake, Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU, Biadia Mtipa, amesema kuwa wakulima wa Nanyamba wako karibu na ukanda wa bahari hali inayosababisha korosho zao kuwa na unyevu mkubwa, jambo linalopunguza ubora na hatimaye kushusha bei sokoni.