Madiwani Nanyamba wahimizwa kufanya mikutano, kusimamia miradi ya maendeleo
1 August 2024, 11:26 am
Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi hivyo ni jukumu la viongozi wa vijiji,Madiwani na watendaji wengine wa serikali katika kusimamia kuhakikisha kuwa miradi hiyo itekelezwa kwa wakati na viwango vinavyotakiwa.
Na Musa Mtepa
Madiwani wa halmashauri ya mji Nanyamba wametakiwa kwenda kwa wananchi na kufanya mikutano ili kuzitambua na kutatua kero zinazo wakabili Pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa July 31,2024 na mkuu wa wilaya ya Mtwara Mwanahamisi Munkunda kwenye kikao cha baraza la kawaida la madiwani la halmashauri ya mji Nanyamba ambapo amesema kuwa serikali kupitia kwa Rais Daktari Samia Suluhu Hassani amepeleka fedha nyingi za miradi katika halmashauri hiyo hivyo ni jukumu kwa madiwani na watendaji wa serikali katika kusimaia utekelezaji wake.
Salumu Issa Chihedile Diwani wa kata ya Nitekela amepokea wito uliotolewa na DC munkunda katika kusimamia miradi ya Maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao huku akisistiza kuwa ni jukumu lao katika kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ubora na kwa wakati.
Kwa upande wake Maliki Majali Diwani wa kata ya Kilomba amesema katika kata yake kuna ujenzi wa Zahanati uliopo katika Kijiji cha Kilomba Chini ambao umefikia katika kiwango cha linta huku halmashauri ikiwa tayari imetenga milioni 50 katika umaliziaji wake huku akisistiza kuwa ukamilikaji wake ni Pamoja na ushirikiano wa nguvu za wananchi.