Jamii FM

Trilioni moja kukuza gesi asilia Mtwara

01/03/2026, 12:53

Mtambo wa uchimbaji Gesi Ardhini ukifanyakazi katika kitalu cha Mnazi Bay Msimbati ikiwa miongoni mwa visima vitatu vinavyotarajiwa kuchimba katika eneo hilo(Picha na Musa Mtepa)

Serikali yawekeza zaidi ya trilioni moja kwenye miradi ya gesi Mtwara, ikilenga kuimarisha upatikanaji wa umeme na kukuza viwanda nchini

Na Musa Mtepa

Ni zaidi ya shilingi trilioni moja za Kitanzania zimewekezwa katika sekta ya gesi asilia kupitia miradi ya uchimbaji katika visima vya Mnazi Bay, Ntorya pamoja na mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Ntorya hadi bomba kuu la Madimba, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini.

Hayo yamesemwa Februari 27, 2026 na Waziri wa Nishati,  Mhe. Deogratius Ndejembi, alipofanya ziara na kuzindua uchimbaji wa kisima kipya cha gesi asilia katika eneo la Mnazi Bay, kata ya Msimbati, wilayani na mkoani Mtwara.

Waziri Ndejembi amesema fedha hizo za Serikali,ni zaidi ya trilioni moja, zinalenga kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa umeme unaotokana na gesi pamoja na kukuza sekta ya viwanda na uzalishaji nchini.

Sauti ya Deogratius Ndejembi, Waziri wa Nishati

Aidha, Waziri Ndejembi amesisitiza kuongeza kasi ya uchimbaji katika maeneo mengine ili vitalu vilivyopo vianze kuzalisha badala ya kubaki kwenye hatua za maandalizi pekee.

Sauti ya Deogratius Ndejembi, Waziri wa Nishati

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja Mradi Mhandisi Coletha Selsi amesema kitalu hicho kinatarajiwa kuongeza zaidi ya futi za ujazo milioni 55 za gesi asilia kwa siku.

Sauti ya Coletha Selsi, Mradi uchimbaji kitalu cha Mnazi Bay

Ameongeza kuwa katika kitalu hicho, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linamiliki asilimia 40 huku M & P ikimiliki asilimia 60. Makubaliano yao yanahusisha uchimbaji wa visima vitatu — viwili vya nyongeza na kimoja cha utafutaji katika shapu jipya la Kasa.

Sauti ya Coletha Selsi, Mradi uchimbaji kitalu cha Mnazi Bay

Ziara hiyo ya siku mbili ya Waziri Ndejembi mkoani Mtwara ilianza Februari 27 na kuhitimishwa Februari 28, 2026. Katika ziara hiyo, alizindua uchimbaji wa kitalu kipya cha Mnazi Bay, kuweka jiwe la msingi mradi wa bomba la gesi kutoka Ntorya kwenda bomba kuu la Madimba, pamoja na kutembelea mradi wa utafutaji wa vyanzo vipya vya gesi katika kijiji cha Hiari (Dangote), unaotekelezwa katika vijiji 40 vya mikoa ya Mtwara na Lindi.