

1 February 2025, 11:41 am
Huu ni utaratibu wa TAKUKURU katika kutoa taarifa kwa umma juu ya matukio mbalimbali yaliyojitokeza katika kila kipindi cha miezi mitatu ya utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kuzuia na kupambana na Rushwa nchini.
Na Musa Mtepa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mtwara imetangaza mafanikio yake katika kuokoa kiasi cha shilingi milioni 253.3 kutoka kwa miradi nane ya maendeleo kati ya 28 ambayo ilikaguliwa.
Katika taarifa aliyotoa kwa waandishi wa habari January 31,2025, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, Bw. Mashauri Elisante, amesema kwamba ukaguzi ulifanyika kwa miradi yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 10.91, na kati ya miradi hiyo, minane ilikutwa na mapungufu katika utekelezaji wake.
Katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2024, TAKUKURU ilikagua miradi mbalimbali katika sekta za elimu, miundombinu, na afya, na kubaini kasoro ambazo zilikuwa zinahitaji kushughulikiwa.
Bw. Mashauri amesisitiza kwamba TAKUKURU ilifanikiwa kuibua kero ya ukosefu wa huduma ya maji katika Kata ya Malatu, wilayani Newala, ambapo TAKUKURU kwa kushirikiana na RUWASA walianzisha mikakati ya kutatua changamoto hiyo, na hatimaye huduma ya maji ilirejeshwa.
Aidha, Bw. Mashauri ameongeza kuwa katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025, TAKUKURU itahakikisha kuwa inazuia vitendo vya rushwa na ubadhirifu katika makusanyo ya mapato ya ndani ya halmashauri, itakagua miradi ya maendeleo kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana, na kuelimisha wananchi kuhusu mapambano dhidi ya rushwa.
Mwisho, ametoa wito kwa wananchi na wadau wote kuendelea kushirikiana katika mapambano ya kupambana na rushwa, na pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha juhudi katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Hii ni taarifa muhimu kutoka kwa TAKUKURU mkoa wa Mtwara kuhusu juhudi zao katika kuimarisha uwazi na kupambana na rushwa katika miradi ya maendeleo.