Jamii FM

RC ,Aomba ridhaa ya CCM kuchukua hatua dhidi ya wahujumu wa Wakulima wa Korosho

14 January 2025, 21:33 pm

Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM katika mkoa wa Mtwara(Picha na RS habari)

Hiki ni kikao cha halmashauri kuu ya chama cha mapinduzi CCM kilicholenga kutoa taarifa za utekelezaji wa ilani pamoja na changamoto zilizojitokeza katika miradi na jamii kwa ujumla

Na Musa Mtepa

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, ameiomba Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara ridhaa ya kuwafuatilia na kuchukua hatua dhidi ya wale wote waliohusika katika kuwahujumu wakulima wa zao la korosho kwa kuwacheleweshea malipo yao na waliosababisha upotevu wa korosho.

Akizungumza kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika Januari 13, 2025, katika ukumbi wa BOT Mtwara, Kanali Sawala amesema kuwa serikali tayari imeanza kuchukua hatua dhidi ya wahusika huku akimuomba Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara kuruhusu hatua zaidi kuchukuliwa ili iwe fundisho kwa wengine.

Sauti ya Kanali Patrick Sawala Mkuu wa mkoa wa Mtwara

Kwa upande wa viongozi wa CCM katika wilaya za Tandahimba na Mtwara Vijijini, Mwenyekiti Nashir Pontiya na Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo, Jafari Mwadili, wamekubaliana na ombi la mkuu wa mkoa na kuonyesha kuunga mkono jitihada hizo za kuchukua hatua dhidi ya wale waliowahujumu wakulima wa korosho.

Sauti ya wenyeviti wa CCM wilaya ya Tandahimba na Mtwara vijiini

Pia, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Newala mji , Yusuph Kanteule, ameonyesha wasiwasi kuhusu wakulima ambao walikuwa wameuza korosho zao mapema lakini hadi sasa hawajalipwa huku akisisitiza kuwa ni muhimu serikali kufuatilia suala hili kwa kina ili wakulima wapewe haki zao na bei waliyoikubali kwenye mnada.

Sauti ya Yusuph Kanteule Mwenyekiti wa halmashauri yam ji Newala

Aidha, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika, Grace Masambaji, amekiri kuwa kumekuwepo na upotevu wa korosho katika baadhi ya AMCOS na kwamba hatua zimeanza kuchukuliwa, huku baadhi ya AMCOS zikianza kurejesha  fedha kwa chama kikuu cha Ushirika cha MAMCU.

Sauti ya Grace Masambaji Mraji msaidizi wa vyama vya ushirika

Hali hii inajitokeza wakati wa msimu wa mavuno wa korosho mwaka 2024/2025, ambapo serikali na viongozi wa CCM wanasisitiza umuhimu wa uwajibikaji na usimamizi bora ili kulinda maslahi ya wakulima na kuhakikisha malipo yao yanatolewa kwa wakati.