Jamii FM

Wananchi wasisitizwa kushiriki kikamilifu uchaguzi serikali za mitaa

26 September 2024, 17:44 pm

Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Mwalimu Hassani Nyange akitoa maelezo ya uchaguzi wa serikali za mitaa(picha na Musa Mtepa)

Uchaguzi wa Serikali za mitaa kote nchini unatarajiwa kufanyika Novemba 27,2024 ambapo kwa mujibu wa kanuni Wakurugenzi wa halmashauri ndio wasimamizi wakuu wa uchaguzi huo.

Na Musa Mtepa

Wananchi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani wametakiwa kushiriki kikamilifu katika michakato ya uchaguzi ili wawe na sifa ya kuchagua na kuchaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.

Wito huu umetolewa leo, Septemba 26, 2024, na Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mwalimu Hassani Nyange, katika kikao cha kutoa maelekezo kwa viongozi mbalimbali kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa, kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Shule ya Sekondari ya Mtwara Ufundi.

Mwalimu Nyange amesema kuwa kujiandikisha katika Orodha ya Wapiga Kura ni hatua muhimu ambayo inawapa wananchi wenye sifa haki ya kisheria kushiriki katika uchaguzi, iwe kama wapiga kura au wagombea katika nafasi za uongozi.

Sauti ya Mwalimu Hassani Nyange Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani

Aidha, Mwalimu Nyange amesisitiza kuwa wananchi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani wenye umri wa miaka 18 au zaidi na wanaokidhi matakwa kisheria wanapaswa kuhamasishwa kushiriki katika uchaguzi, aidha kwa kuchagua au kuchaguliwa.

Sauti ya Mwalimu Hassani Nyange Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani

Mwanahamisi Libubulu, Diwani wa Viti Maalumu (CCM) Manispaa ya Mtwara Mikindani, na Saidi Issa Kulaga, Katibu wa Chama cha CUF wilaya ya Mtwara, wamesema wamepokea maelekezo haya kwa mikono miwili na kwamba ni wajibu wao kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa.

Sauti ya Mwanahamisi Libubulu Diwani Viti maalum(CCM) na Saidi Kulaga katibu wa CUF wilaya ya Mtwara.

Nao Viongozi wa dini  wamesisitiza umuhimu wa serikali kutoa elimu juu ya umuhimu wa wananchi kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa, kwakuwa  huduma mbalimbali zinaanzia kupatikana kupitia viongozi wa chini wa mitaa na vitongoji.

Sauti ya viongozi wa Dini wakizungumzia maelekezo
Baadhi ya Wananchi waliojitokeza katika maelekezo ya uchaguzi yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani(Picha na Musa Mtepa)