Zoezi la ugawaji vitambulisho vya NIDA lazinduliwa
28 October 2023, 14:10 pm
Wananchi wote ambao hawajasajiliwa kufika kwenye ofisi hizo kwa ajili ya kupata utaratibu awali kwa ajili ya kusajiliwa ili na wao waweze kupata vitambulisho hivyo kama wengine
Na Musa Mtepa;
Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Ahmadi Abasi, Oktoba 27,2023 amezindua zoezi ugawaji wa vitambulisho vya Taifa NIDA 300,149 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mh Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Daktari Samia Suluhu Hassani la kuitaka mamlaka ya vitambulisho taifa NIDA kuhakikisha wanawapatia vitambulisho Wananchi wanaoishi mikoa ya pembezoni.
Akizindua zoezi hilo katika viwanja vya kata ya ufukoni Manispaa ya Mtwara Mikindani Kanal Ahmed Abasi ameipongeza mamlaka ya Vitambulisho NIDA kwa utekelezaji wa haraka Maagizo hayo huku akiwataka watendaji wa kata, mitaa na vijiji ambao walimepewa dhamana ya kugawa vitambulisho hivyo kuhakikisha wanazingatia kanuni, sheria na taratibu za utumishi wa umma katika kutekeleza jukumu hilo ili kuwafikia wananchi kwa uharaka.
Pia RC Ahmed Abasi amewataka wanaopata vitambulisho hivyo kuvitunza ili viweze kuwasaidia katika mahitaji mbalimbali ambayo sasa ili uyapate ni lazima uwe na aidha kitambulisho chenyewe au namba yake.
Nae Bw Gide Magile afisa usajili kutoka mamlaka ya vitambulisho vya taifa NIDA mkoa wa Mtwara amewaomba Wananchi wote ambao walifanya usajili hapo awali na kutopata vitambulisho vya taifa kujitokeza katika ofisi za kata, mitaa na vijiji vilikopelekwa kwa ajili ya kuwagawia.
Aidha Bw Magile amewataka wananchi wote ambao hawajasajiliwa kufika kwenye ofisi hizo kwa ajili ya kupata utaratibu awali kwa ajili ya kusajiliwa ili na wao waweze kupata vitambulisho hivyo kama wengine.
Kwa upande wake Bi Sada Saidi Dalli Mwananchi wa kata ya ufukoni ameipongeza serikali kwa kitendo cha kuwapatia vitambulisho kwasababu ni muda mrefu wananchi walikuwa wakivihitaji bila mafanikio hivyo kwa kitendo kilichofanywa na serikali kuwaletea katika ofisi za kata, mitaa na vijiji vimerahisisha upatikanaji na kuondoa kero ya kusafiri umbali mrefu.
Pia Bi Sada amesema kupata kwa vitambulisho hivyo vitamsaidia kuondoa usumbufu aliokuwa akiupta hapo awali alipokuwa akihitaji huduma kwa baadhi ya ofisi kitendo ambacho kilikuwa kikimnyima haki yake ya msingi.