DANGOTE kupiga tafu miradi ya Milioni 648 Mtwara Vijijini
28 February 2021, 10:14 am
Kiwanda cha saruji DANGOTE Mtwara tarehe 26 Februari, 2021 kimeingia makubaliano maalum na halmashauri ya wilaya ya Mtwara kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye thamani ya milioni 648 katika sekta ya elimu, afya, maji na michezo.
Makubaliano hayo yamefanyika katika ofisi za makao makuu ya halmashauri zilizopo kata ya mkunwa huku yakishuhudiwa na wakuu wa idara na vitengo kutoka pande zote mbili ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera inayomtaka mwekezaji kuchangia utekelezaji wa miradi inayotoa huduma kwa jamii yaani CSR (Cooperate Social Responsibility).
Akiongea mara baada ya kutiliana Saini makubaliano hayo, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara Bi. Erica E. Yegella, ameishukuru kampuni ya DANGOTE kwa kuonesha nia thabiti ya kushirikiana na Serikali kupitia uboreshaji wa miradi ya huduma za jamii jambo ambalo litasaidia kuimarisha mahusiano baina ya mmwekezaji, serikali na jamii.
Ameendelea kusema kuwa miradi inayoenda kutekelezwa ni ile ambayo ipo katika utekelezaji wa mpango wa bajeti hii inayoendelea ya mwaka wa fedha 2020/2021 ambapo kuna baadhi ya shule, zahanati zilizo katika hatua tofauti za ujenzi zitaweza kumaliziwa na kuanza kutoa huduma, kuchimba visima vya maji katika maeneo tofauti Pamoja na kuboresha sekta ya michezo.
Kwa upande wa uongozi wa kiwanda hicho kupitia afisa mahusiano ya jamii Bwn. Siraji Nalikane, ameishukuru sana serikali kwa kuweka utaratibu nzuri utakaoimarisha mahusiano, pia amekiri kuwa makubaliano haya yamefikiwa kihalali kabisa baada ya pande zote mbili kukaa na kujadiliana vigezo na masharti ya kuzingatiwa juu ya miradi inayotakiwa kutekelezwa kulingana na vipaumbele vya serikali kwa mwaka husika.
Bwana Nalikane ameongeza kuwa, makubaliano haya yanaenda kuongezea nguvu kwenye miradi iliyoanza kutekelezwa na kupitia uongozi wa kiwanda chao chini ya Bw. Balla ana uhakika jambo hili litatekelezwa kwa umakini ili kupata ubora na matokeo yatakayoimarisha uhusiano uliopo, ametanabaisha kwa sasa kuna baadhi ya miradi iliyoanza kutekelezwa kama vile ujenzi unaoendelea wa shule ya msingi Hiari.
Credit: Afisa Habari – Isaac Bilali
Matukio katika picha