Jamii FM
Jamii FM
27 October 2025, 21:38 pm

Mgombea Ubunge wa Mtwara Vijijini kupitia CUF, Shamsia Azizi Mtamba, amewataka wananchi wa Kata ya Madimba kuendelea kumuamini na kumpa kura, akiahidi kuendeleza maendeleo na kulinda kura zao dhidi ya propaganda za kisiasa
Na Musa MtepaMtwara–Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini anaetetea nafasi hiyo kupitia tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Shamsia Azizi Mtamba, amewaomba wananchi wa Kata ya Madimba kutokufanya kosa la kumchagua mgombea mwingine zaidi yake.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo, Oktoba 27, 2025, katika Kijiji cha Madimba, Shamsia amewataka wananchi hao kuendelea kumuamini ili aweze kuendeleza juhudi za kuleta maendeleo katika kata hiyo.

Aidha, Shamsia ametumia nafasi hiyo kuwatoa hofu wananchi wa Madimba akisema kuwa amejipanga kulinda kura zake, huku akiwataka wananchi kupuuza propaganda zinazoenezwa na baadhi ya wanasiasa ya kuwa hata akishinda hatotangazwa.
Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Madimba kupitia tiketi ya CUF, Bashiru Mchamba, amewaomba wananchi wampe kura ili aweze kushirikiana nao katika kuleta maendeleo na ustawi wa kata hiyo.

Wakizungumza kuhusu mwenendo wa kampeni, baadhi ya wananchi wa Kata ya Madimba wamesema baadhi ya wagombea wameonyesha kugusa changamoto zinazowakabili, zikiwemo miundombinu ya barabara, huduma za afya, elimu na upatikanaji wa maji safi.
