Mtwara waweka Mikakati ya Kupunguza vifo vya Mama Wajawazito
24 March 2022, 12:29 pm
Na Gregory Millanzi.
Mikakati mingine iliyowekwa na Mkoa ili kuhakikisha inapunguza vifo vitokanavyo na uzazi ni kuhakikisha gari la kubeba Wagonjwa (Ambulance) katika vituo vya afya na Hospitali zinafanya kazi muda wote ili kuimarisha mfumo wa Rufaa kutoka ngazi ya Familia hadi Hospitali.
Dkt Mohamed Kodi – Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara
Mkoa wa Mtwara umeamua kuweka Mipango Mikakati ya Kudhibiti vifo vitokanavyo na uzazi kwa Mama Mjamzito, lengo ni kuhakikisha tatizo hilo linaisha na linabaki kuwa Historia.
Akizungumza na Jamii FM Radio Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Dkt Mohamed Kodi amesema, vifo vya akina Mama wajawazito vimeendelea kupungua japo siyo kwa kasi inayotarajiwa kutoka vifo 62 Mwezi Januari mpaka Oktoba Mwaka 2020 hadi kufika vifo 60 mwaka 2021 kwa kipindi husika, katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2021 vilitokea vifo 13 ambayo ni pungufu ukilinganishwa na Julai hadi Septemba 2020 ambapo vifo vilikua 16.
Dkt Kodi amesema kuwa wameamua kuweka mikakati ya kupunguza vifo vitokakanvyo na uzazi kwa Mama wajawazito ili kuweza kunusuru maisha ya Mama na Mtoto , ambapo kwa kipindi cha Januari mpaka Oktoba 2021 Jumla ya wajawazito 34,239 walijifungua, kati yao 1,176 ambao ni sawa na asilimia 3.4 walijifungulia Nyumbani, ikilinganishwa na asilimia 4.04 ya Januari mpaka Oktoba 2020.
Dkt Kodi amesema kuwa Idadi ya Wajawazito 1,830 walikuwa na Matatizo wakati na baada ya kujifungua, kati yao 1,066 amnbao ni sawa na asilimia 58.3 tatizo kubwa lilikuwa uzazi pingamizi, Wajawazito 4,335 kati ya 31,973 sawa na asilimia 15 waliojifungulia vituoni walihitaji huduma za dharura za upasuaji.
Ameongeza kuwa Mikakati ya Kupunguza vifo vitokananvyo na uzazi ni pamoja na Kuanzisha kanzidata itakatofuatilia Mama Njamzito tangu anapokelewa wodini hadi kujifungua, kuendelea kutoa Elimu ya afya kwa Jamii juu ya Umuhimu wa Mama wajawazito kuwahi kuanza kliniki pindi wanapojihisi kuwa na ujauzito na kujifungulia kwenye kituo cha kutolea huduma.
Mikakati mingine iliyowekwa na Mkoa ili kuhakikisha inapunguza vifo vitokanavyo na uzazi ni kuhakikisha gari la kubeba Wagonjwa (Ambulance) katika vituo vya afya na Hospitali zinafanya kazi muda wote ili kuimarisha mfumo wa Rufaa kutoka ngazi ya Familia hadi Hospitali.
Kuendelea kutumia teknolojia ya Mawasiliano (WhatsApp Groups) ambapo akitokea Mama au mtoto mwenye shida watoa huduma hupata Msaada wa kitaalamu kutoka kwa Madaktari bingwa. Pia Mkoa umepanga Kuimarisha kasi ya ukusanyaji Damu salama kwenye Halmashauri ili kupunguza vifo vitokanavyo na ukosefu wa damu kwa akina mama wanaotokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua .
Baadhi ya Wadau wa Afya Mkoa wa Mtwara wamepongeza juhudi hizo ambazo zinaonyesha jitihada za mkoa kutatua na kufatilia kwa ukaribu tatizo la vifo vya Mama wajawazito, Rehema Sadiki Mkazi wa Majengo Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, ameipongeza Serikali ya Mkoa kwakuhakikisha wanawajali wanawake hasa wajawazito.
“Mimi ni mama wa watoto watatu, watoto wangu waote nimejifungulia kijijini na hali ilikuwa ngumu kupata huduma sahihi kwa wajawazito hasa wakati wa kujifungua, wakati mwingine nilikuwa nashuhudia wajawazito wanaangaika na wanahatarisha maisha yao kutokana na mazingira, ila kwa sasa Rais Samia amehakikisha tunajifungua kwa hali ya usalama na kunusuru maisha ya Mtoto” Rehema Sadiki.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara amewasihi wananchi kufuata hatua sahihi na maelekezo ya watoa huduma za Afya ili kuhakiksha wanaepuka matatizo ya kiafya yanayosababisha vifo, pia amewaasa watoa huduma za afya kuwa karibu na Wananchi ili kujua matatizo yao na kama yanaweza kutatuliwa kwenye maeneo yao basi yafanyike na kama yanashindika yapelekwe sehemu husika kwa utatuzi zaidi.