Wawezeshaji TASAF wasisitizwa kutumia weledi uibuaji miradi
24 February 2021, 04:45 am
Timu ya wataalamu wa sekta mbalimbali halmashauri ya wilaya mtwara imeendelea na mafunzo ya siku sita yatakayowawezesha kusaidia uibuaji wa miradi ya kipindi cha ari kwa walengwa wa kaya maskini kupitia mradi wa TASAF kunusuru kaya maskini awamu ya tatu sehemu ya pili unaoendelea katika jumla ya Vijiji 57.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo na ubunifu wawezeshaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini kutoka sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, ujenzi, mazingira, afya, ardhi ambapo mara baada ya mafunzo watajikita vijijini kwaajili ya kuwasaidia walengwa kuibua miradi itakayowawezesha kujiongezea kipato kwa kipindi chote cha hali ngumu.
Akiongea na waandishi wa habari wakati wa mafunzo hayo, mmoja wa wawezeshaji ngazi ya halmashauri Bwana Hassan Dadi ametanabaisha kuwa, mara nyingi elimu wanayopata inasaidia katika kuibua miradi yenye tija kwa walengwa, kutokana na mbinu shirikishi zinazotumika kuwaandaa walengwa kutambua umuhimu na faida ya miradi.
Ameendelea kusema kuwa elimu wanayoipata hapa inawataka kuongeza weledi na ubunifu mkubwa kwa kuwa miradi yote itakayoibuliwa na kutekelezwa na walengwa inatakiwa kufikishwa kwao kupitia elimu ya uhamasishaji ili kupata washiriki wenye morali na kazi.
Credit: Afisa habari – Isaac Bilali