Mila, desturi kikwazo wanawake kuwa viongozi
21 June 2023, 13:40 pm
Mila na tamaduni zinachukua nafasi kubwa katika kuenzi nafasi za wazee katika jamii zetu, wandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kupunguza baadhi ya mila zenye kuharibu jamii hasa wanawake.
Na Musa Mtepa
Wandishi wa habari mkoani Mtwara wameelezea changamoto zinazowasababishia wanawake wengi kutojihusisha katika nyadhifa mbalimbali za uongozi huku sababu ikielezwa kuwa utamaduni na imani ya dini ndio kikwazo kikubwa.
Wakizungumza baada ya mafunzo ya siku mbili Juni 19-20, 2023 yaliyohusu kumwezesha mwanamke kuingia na kujihusisha kwenye uongozi katika jamii chini ya shirika lisilo la kiserikali la Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), wamesema kuwa mila, desturi na imani ndio kikwazo kikubwa kwa wanawake wa mkoa wa Mtwara kutojihusisha na masuala ya uongozi.
Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo Bw. Deogratus Temba amesema kutokana na majadiliano wamebaini kuwa baadhi ya mila na desturi zinazofanyika katika jamii hupelekea mwanamke kutoshiriki katika nyazifa za uongozi na wakati mwingine jamii hujenga taswira ya mwanamke kumweka kuwa dhaifu katika jamii.