Wanufaika wa TASAF Mtwara watakiwa kutumia vizuri elimu ya akiba na mikopo
18 February 2021, 10:20 am
Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Bi. Zuena G. Myula leo tarehe 17 Februari, 2021 amewataka walengwa wa kaya maskini kuendelea kukutana katika vikundi vyao kwa minajili ya kupeana elimu ya akiba na mikopo pamoja na kufanya marejesho ya fedha kwa wale wote waliokopa ili kuhuisha matarajio yao.
Ameyasema hayo wakati wa zoezi la ufuatiliaji wa malipo ya walengwa wa kaya maskini yanayoendelea katika vijiji 57 huku akiendelea kuwasisitiza kuchukua fedha na kufanya matumizi ya msingi yenye kuleta mafanikio kwa kaya zao.
Aidha, Bi. Zuena amewaagiza walengwa hao kusimama kidete kuhakikisha wategemezi wanaotakiwa kuwa masomoni wanafanya hivyo kwa wakati ili kuepuka adha ya migogoro ya kisheria inayoweza kuwakumba mara ukaguzi wa kubaini watoro utakapoanza.
Juu ya hapo, amewakumbusha walengwa kuzingatia kanuni na taratibu za TASAF kwa kipindi chote mradi utakapofanya kazi kwakuwa kuna fursa nyingi ambazo Serikali inaendelea kuzitoa kwa kaya za walengwa zenye lengo la kuwakomboa kiuchumi huku akitaja mfano nzuri hivi karibuni zaidi ya watoto 80 kutoka katika kaya hizo wamefanikiwa kupata ufadhili wa kusoma fani mbalimbali katika chuo cha maendeleo ya Wananchi Masasi (FDC).