Jamii FM

WAJAWAZITO LIKOMBE WAENDELEA KUONWA, WAPOKEA VIFAA VYA KUJIFUNGULIA KUTOKA PLATINUM

17 November 2022, 16:52 pm

Na Gregory Millanzi

Kampuni ya Utoaji wa mikopo ya Platinum Novemba 10,2022 imekabidhi vifaa tiba vya kujifungulia vyenye thamani ya shilingi milioni sita( 6,000,000) kwa Kituo cha afya cha Likombe kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani ili kusaidia kutatua changamoto wanazokabiliana nazo akina mama wajawazito wakati wa kujifungua.

Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Dunstan Kyobya ameipongeza Kampuni ya PLATINUM kwa kujitoa kwao na kuisadia jamii kwa kutoa vifaa tiba kwa akina mama wajawazito.

Aidha Mkuu wa Wilaya amewasisitiza watumishi wa Kituo cha afya Likombe kuhakikisha wanavitunza vifaa hivyo ili viweze kufanya kazi kwa muda mrefu, kuwahudumia akina mama wengi zaidi Pamoja na na kupunguza changamoto zilizopo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani COL. Emanuel Mwaigobeko ameishukuru Kampuni hiyo kwa kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kutoa vifaa tiba ambavyo kwa kiasi kikubwa vinaenda kusaidia kupunguza mzigo kwa serikali na ametoa wito kwa Makampuni na Taasisi nyingine za biashara kuona umuhimu wa kusaidia jamii kwenye kila faida wanayoipata.

Asha Hamis mkazi wa Majengo Mtwara mjini amesema kuwa, vifaa hivyo vimekuja kwa muda muafaka sana kwasababu kituo hicho cha afya kwa sasa kinasaidia na kuhudumia wakazi wengi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani na hata waliopo Vijijini, na uwepo wa vifaa hivyo vitasaidia watoa huduma kufanya kazi kwa ufanisi na kuokoa maisha ya Mama na mtoto.

” Mimi niliwahi kuleta mwanangu hapa kujifungua na niwapongeze sana watoa huduma wa kituo hiki maana walimuhudumia vizuri binti yangu na wakafanikisha kuokoa maisha ya Mama na mtoto na kwa sasa wanaendelea vizuri na anahudhuroa kliniki hapa hapa” amesema Asha Hamis.

Nae Mwajuma Juma amesema kuwa kuongezeka kwa vifaa tiba hivyo vitafanya huduma za kituo hicho cha Likombe kuwa na idadi kubwa zaidi ya kina mama wajawazito kutoka kila kona na amewaomba wadau wengine kujitokea zaidi vifaa.

” Sisi kina mama wajawazito huwa tunasimuliana uko mtaani kuwa kituo fulani cha afya kina huduma nzuri na ni salama kwa kunusuru maisha ya mama na mtoto, na hapo ndio tunaenda kujifungua kwenye hicho kituo, kwasasa mtaani kituo ambacho ni salama kwa maisha ya mama na mtoto wakati wakujifungua ni hapa Likombe kwasababu vifaa vipo na huduma nzuri inapatikana” amesema Mwajuma Juma mkazi wa Magomeni Mtwara.

Meneja wa Kampuni ya Platinum Bwana Richard Manyaga amesema kuwa Kampuni yao imetoa vifaa tiba baada ya kuona kuna changamoto kubwa ambazo akina mama wanakutana nazo wakati wa kujifungua .

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na vitanda vya kujifungulia viwili, magodoro mawili, Vifaa vya kujingulia (mama delivery Kit) , mashine ya kupimia mapigo ya mtoto, mashine ya kutakasa vifaa (auto clave) Pamoja na vifaa vingine.