Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi yafanya kikao na Wadau wa Uchaguzi Mkoani Mtwara
17 January 2025, 10:52 am
Hii inalenga kutoa elimu ya ujiandikishaji na hamasa kwa Wananchi kushiriki katika zoezi la kujiandikisha na uboreshaji wa taarifa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura linalotarajiwa kufanyika hivi karibuni katika mkoa wa Mtwara.
Na Mwanahamisi Chikambu
Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) , Januari 16, 2025, imefanya kikao cha kujumuisha wadau mbalimbali wa uchaguzi mkoani Mtwara, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), tawi la Mtwara, na kilihusisha viongozi wa dini, vyama vya siasa, wawakilishi wa wazee wa kimila, watu wenye ulemavu, vijana, wanawake, asasi za kiraia, wahariri na waandishi wa habari.
Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi, Jaji Jacobs Mwambegele, amesema kuwa lengo kuu la mkutano huo lilikuwa kutoa taarifa kuhusu zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na jinsi zoezi hili litakavyofanyika katika vituo vya kujiandikisha.
Aidha amewaomba viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kuhakikisha wananchi wanahamasika na kujiandikisha kwa ufanisi.
Katika taarifa iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Ramadhani, imebainishwa kuwa idadi ya wapiga kura wanaotarajiwa kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura ni 5,586,433, sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura 29,754,699 waliopo katika daftari la kudumu baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka 2019.
Kwa taarifa zaidi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kujiandikisha ili kuhakikisha kuwa na uchaguzi wa haki na usawa mwaka huu.