Biteko awasha umeme wa REA Mtwara
16 November 2023, 13:13 pm
Na Grace Hamisi
Naibu Waziri mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko Novemba 15,2023 amewasha umeme wa ujazilizi katika maeneo ya vijiji – miji awamu ya III mitaa ya Pachoto A, Pachoto B na Pwani kata ya Naliendele mkoani Mtwara.
Sambamba na hilo amewapongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kusimamia vyema kazi ya kusambaza umeme, amewataka kutokucheka na wakandarasi hao ili kazi ya kupeleka mahitaji ya umeme kwa wananchi ifanyike kwa ufanisi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA, Jones Olotu alimweleza Naibu Waziri Mkuu kuwa, Mkoa wa Mtwara umetengewa shilingi bilioni 170 kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini na kwamba katika vijiji 785 vya mkoa huo, Vijiji 401 bado havina umeme lakini wakandarasi kampuni ya Derm, Central na Namis wanaendelea kusambaza umeme kwenye Vijiji vilivyosalia.
Hata hivyo Naibu Waziri mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amezitaka kampuni zinazosimamia miradi ya umeme nchini Tanesco na Wakala wa Nishati vijijini (REA) kununua vifaa vya umeme vinavyozalishwa hapa nchini ili kukuza viwanda vya ndani, kuvipa thamani na kukuza ajira pamoja na uchumi wa Nchi.