Jamii FM

INEC yawataka maafisa kuzingatia sheria, maadili

16 July 2025, 11:26 am

Balozi Omari Ramadhani Mapuri akifungua mafunzo kwa waratibu na wasimamizi wa uchaguzi wa mikoa ya Lindi na Mtwara yaliyofanyika ukumbi wa mikutano wa BOT mjini Mtwara(Picha na Musa Mtepa)

“Maafisa wa uchaguzi wametakiwa kufuata misingi ya kikatiba na kisheria ili kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki,” amesema Balozi Mapuri, katika mafunzo yaliyofanyika Mtwara yakiongozwa na INEC Julai 15, 2025

NA Musa Mtepa

Maafisa wa usimamizi wa uchaguzi wametakiwa kufuata hatua na taratibu mbalimbali za kikatiba na kisheria ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa mujibu wa malengo na matarajio ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Kauli hiyo imetolewa Julai 15, 2025 na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Balozi Omar Ramadhani Mapuri, wakati akifungua mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara, yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Mtwara.

Balozi Mapuri amesema kuwa, kwa mujibu wa Kifungu cha Sheria 20(2) ya mwaka 2024, mtumishi yeyote aliyeajiriwa, kuteuliwa au kuazimwa na Tume kwa kipindi anapotekeleza majukumu ya Tume, atachukuliwa kuwa ni mtumishi wa Tume. Hivyo, amewataka wote walioteuliwa kuzingatia misingi, maadili na taratibu zinazoongoza kazi za Tume hiyo.

Sauti ya 1: Balozi Omar Ramadhani Mapuri – Mjumbe wa INEC

Aidha, Balozi Mapuri amewataka wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha wanazingatia viapo vyao vya kutunza siri, kujitolea kwa uadilifu, na kuepuka kuwa wanachama wa vyama vya siasa katika kipindi chote cha uchaguzi.

Sauti ya 2: Balozi Omar Ramadhani Mapuri – Mjumbe wa INEC

Kwa upande wake, Bi Giveness Aswila, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, amewapongeza washiriki wa mafunzo hayo kwa kuchaguliwa kushiriki jukumu hilo muhimu na kuwasisitiza kuwa ni wajibu wa kila mmoja wao kulinda heshima ya nafasi waliyopewa ili wasivuruge sifa na uaminifu wao binafsi.

Sauti ya 3: Bi Giveness Aswila – Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa INEC